Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Viambajengo vya Nadharia ya Naratolojia

February 27th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

NADHARIA ya simulizi hujikita katika kipengele cha wakati ambacho huangaliwa kwa kuvichunguza vigezo kama vile:-

  1. mpangilio
  2. muda na
  3. idadi marudio

Mpangilio – Katika kigezo hiki, matukio huweza kusimuliwa katika mfuatano wa kiwakati ama kwa kutofungamana yanaposimuliwa kiwakati, msuko na hadithi huwa na mpangilio sawa.

Muda – Kigezo hiki hujikita katika uhusiano katika hadithi na kipindi ambacho kimechukuliwa, kipindi kirefua u kifupi? Muda katika nadharia ya naratolojia hujitokeza katika jinsi tano;-

Muhtasari –  ambapo muda wa usemi au matini yaani usomaji unachukuliwa kuwa mfupi kushinda ule wa hadithi. Kwa mujibu wa Rimmon-Kenan kasi ya hadithi huharakishwa katika muhstasari unaotokana na ufupishwaji wa muda fulani kwa kauli chache.

Udondoshaji – Hii ni dhana nyingine ambayo hurejelea pale mabapo maelezo fulani yameachwa katika matini fulani, ilhali hadithi yenyewe ina wakati fulani. Katika hali hii wakati hadithi na wakati matini huwa tofauti.

Onyesho ni dhana ambayo huleta sifa ya uigizaji katika matini yoyoyte ile.

Idadi marudio au umara – Katika dhana hii wahakiki wa naratolojia hurejelea mara ambazo matukio hutokea katika hadithi au mara ngapi matukio hayo yanasimuliwa.

Wananaratolojia wamebainisha aina tatu za urudiaji kama vile, tukio lililotokea mara moja linaweza kusimuliwa mara moja, pia tukio lenyewe laweza kusimuliwa mara kadha na panakuwa na urudiaji wakisimulizi na hatimaye tukio likitokea mara kadhaa linasimuliwa mara moja.

Uhakiki wa kinaratolojia huwaangalia wahusika kama kipengele muhimu cha matini ya kifasihi.

Katika kuwabainisha wahusika, kuna uelezaji wa moja kwa moja ambapo maelezo ya wazi wazi kumhusu mhusika yanatolewa na mwandishi. Kwa mfano katika ‘Rosa Mistika’ maelezo kuhusu yanatolewa waziwazi na mwandishi. Katika uwasilishaji usio wa moja kwa moja unahusisha matendo ya wahusika, maneno yao, mandhari au hali zao.

Msomaji huangalia jinsi wahusika wamewasilishwa na mandishi na kuwatambua. Kipengele kingine cha uhakiki huu ni mtazamo wa mhakiki au mtambaji. Mwandishi huwa na mtazamo fulani kuhusu maswala kadhaa na ambao labda angetaka amshirikishe msomaji.

Nadharia ya naratolojia inahusiana na mwelemeo wake mkuu kwenye muundo wa kazi bila kuhusisha na muktadha wa kihistoria, kijamii, kisiasa au kitamaduni wa kazi zenyewe.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong’o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.

Wellek Rene & Austin Warren ( 1986). Theory of Literature. Harmondworth: Penguin