Habari za Kitaifa

Ukuruba wa Raila na Ruto wazua tumbojoto Mlimani

May 27th, 2024 3 min read

Na LUCAS BARASA

UKURUBA wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga unaonekana kumsukuma pembeni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua serikalini, siasa za uchaguzi wa 2027 zikionekana kuanza kushika kasi.

Bw Gachagua mnamo wikendi aliwaonya baadhi ya wanasiasa kutoka Bonde la Ufa dhidi ya kuingilia siasa za Mlima Kenya akisema viongozi kutoka eneo hilo wanajipanga wenyewe.

Uhusiano kati ya Bw Odinga na Rais Ruto ulianza kudhihirika wazi mnamo Februari 24 pale viongozi hao walipokutana nyumbani kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na tangu wakati huo Bw Gachagua ameonekana kuyumbishwa kisiasa.

Mkutano kati ya Rais na Raila ulifanyika baada ya serikali kutangaza kuwa inaunga mkono azma ya Bw Odinga ya kutwaa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Tangu wakati huo, Bw Odinga amekuwa akikutana na baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini na hata wiki jana alimuaga Bw Museveni ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili nchini humu.

Urafiki huu kati ya Rais na Bw Odinga umesababisha baadhi ya wanasiasa wa Upinzani waliokuwa wakosoaji wakubwa wa serikali, kufyata ndimi zao.

Baadhi yao, kama vile Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga na Kiongozi wa Wachache Bungeni, Opiyo Wandayi, hata waliandamana na Rais kwenye ziara yake ya wiki moja nchini Marekani.

Ni urafiki huu ndio umemsukuma Bw Gachagua kando huku akionekana kutokuwa na ushawishi wowote ndani ya serikali ikilinganishwa na Raila.

Naibu wa Rais anadai kuwa kuna wanasiasa ambao wanampiga vita kutoka Bonde la Ufa huku ‘Mlima ukiporomoka’.

Pia ushirikiano wa Rais na Raila umemkosesha mbinu ya kumvamia kiongozi huyo wa ODM kwa maneno makali jinsi alivyokuwa akifanya hapo awali.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Prof Nyaga Kindiki, itakuwa rahisi sana kwa Rais kumtema Bw Gachagua 2027 iwapo Bw Odinga atafanikiwa kupata kazi ya AUC.

“Raila huenda hatakuwa na haja tena na urais na atarudi ngome yake ya kisiasa ya Nyanza na kuwashauri wakazi wamuunge mkono Dkt Ruto. Iwapo Rais atakuwa akidhibiti siasa za Nyanza na Magharibi, atachaguliwa kwa urahisi sana hata akimtema Bw Gachagua,” akasema Prof Nyaga katika mahojiano na Taifa Leo.

Licha ya Bw Odinga kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Magharibi, Rais Ruto tayari pia amewatia kapuni vigogo wa siasa kutoka eneo hilo.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ni viongozi wakuu katika utawala wa sasa wanaotoka Magharibi.

Rais Ruto amerusha chambo zaidi Magharibi kwa kumpa seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malala wadhifa wa katibu wa UDA.

Kakamega ambayo inajivunia idadi kubwa ya wapigakura baada ya Kiambu pia huenda ikamkumbatia Rais kama ataendelea kushirikiana na Raila kwa sababu ODM ndiyo hutamba kisiasa gatuzi hilo.

“Kile ambacho Bw Gachagua alisahau baada ya kuahidi kumzima Bw Odinga kuingia ikulu ni kuwa Rais huwa wa Wakenya walio ndani na nje ya serikali,” akaongeza Prof Nyaga, nduguye Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki.

Licha ya masaibu hayo, wandani wa Bw Gachagua nao wameshikilia kuwa anastahili heshima ndani ya serikali kutokana na uungwaji ambao UDA ilipata Mlima Kenya hadi ikaunda serikali.

“Tuliamka mapema kuwachagua Rais na naibu wake. Ruto alidhalilishwa sana akiwa naibu rais na hatutaruhusu mtoto wetu Gachagua atendewe hivyo. Yametosha,” akasema Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga.

Akionekana kama aliyeweka mikakati ya kujilinda kisiasa, Bw Gachagua naye amewafikia wanasiasa kutoka Upinzani wanaotoka Mlima Kenya akilenga kuweka eneo zima “nyuma yake”.

Mwenyekiti wa Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga Muriithi King’ara amemtaka Bw Gachagua asitikiswe kwa kuwa yeye ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya akisema eneo hilo litaungana nyuma yake.

Baadhi ya wakazi wanahofia kuwa Bw Gachagua akitengwa, juhudi zake za kumaliza janga la pombe haramu, uraibu wa dawa za kulevya na ufufuzi wa sekta za majani chai, kahawa na maziwa hazitafua dafu.