DimbaUncategorized

Cheche aomba mashabiki wajitokeze kwa wingi Junior Starlets wakikafunga dhidi ya Uganda

Na TOTO AREGE March 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KOCHA Mildred Cheche wa Junior Starlets amesema hawatalaza damu watakapovaana na Uganda Teen Cranes kwa mechi ya marudiano katika raundi ya pili ya mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la mabinti wasiozidi miaka 17.

Mechi hiyo itagaragazwa Jumapili katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi kuanzia saa tisa alasiri.

Kenya inaongoza kwa jumla ya magoli 2-0 kutokana mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa Jumamosi 8 mwezi huu katika Uwanja wa Nakivubo Hamz jijini Kampala, Uganda.

Mshambuliaji Edinah Nasipwondi alifunga bao la kwanza dakika ya 36, kabla ya mshambuliaji Joan Ogola kufunga bao la pili dakika ya 46 ya muda wa ziada kipindi cha kwanza.

“Lazima tuzuia kufungwa magoli nasi tufunge ya kwetu ili kuhakikisha ushindi mnono nyumbani. Uganda ni tishio kwani wanaweza pia kupiga makombora ya kutoka umbali. Lengo letu ni kunogesha tena Kombe la Dunia mara ya pili,” alionya kocha Cheche.

Mshambuliaji Edinah Nasipwondi (kushoto) wa Junior Starlets na beki Shamirah Namukabirye wa Uganda Teen Cranes wakifuata mpira wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza jijini Kampala, Uganda. PICHA | FKF

Kenya, ambayo haijashindwa nyumbani, itacheza Nyayo kwa mara ya kwanza. Mechi yao ya mwisho nyumbani ilikuwa dhidi ya Ethiopia Mei 19 mwaka jana katika uga wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, ambako walifuzu kwa Kombe la Dunia kufuatia ushindi wa 3-0 wa jumla ya mabao.

Cheche aliandikisha historia kuwa kocha wa kwanza kuipeleka timu yoyote ya Kenya katika Kombe la Dunia mwaka jana, dimba hilo la U17 lilipoandaliwa katika Jamuhuri ya Dominica.

Nyayo ni uwanja wa pili kwa ukubwa nchini unaoweza kusitiri mashabiki 30,000 na umekuwa ukifanyiwa ukarabati tangu 2023.

Timu ya taifa ya Kenya ya soka ya wanawake Harambee Starlets ndiyo iliyotumia uwanja huo mara ya mwisho mnamo Novemba 19, 2023 dhidi ya Botswana katika mechi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) huku mechi ikiisha kwa sare ya 1-1 kwa jumla.

Hata hivyo, Cheche ameomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa timu sapoti.

“Kucheza mbele ya mashabiki na familia zetu itakuwa ni fahari kwetu.  Sapoti kubwa ya Wakenya huongeza morali. Tunawaahidi waje kwa wingi hatutawaangusha,” alisema Cheche ambaye ana leseni ya ukocha ya CAF A.

Nahodha Halima Imbachi anaelewa umuhimu wa kumaliza kazi nyumbani.

“Tunafahamu mechi ya Jumapili ni muhimu. Kucheza nyumbani kunaturuhusu kuwa watulivu, tofauti na wapinzani wetu ambao watakuwa chini ya shinikizo la kufunga,” alisema Imbachi, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere katika Kaunti ya Kakamega.

Imbachi, ambaye alimrithi Elizabeth Ochaka kama nahodha, pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Kombe la Dunia mwaka jana.

Kikosi

Kocha Cheche hatarajiwi kufanya mabadiliko katika kikosi kutokana na kikosi kilichocheza dhidi ya Uganda, licha ya kukosa nafasi za kufunga mapema katika dakika 30 za kwanza za mechi.

Velma Abwire huenda atakuwa golini, akilindwa na mabeki Lorine Ilavonga, Jenevive Mithel, Judith Nandwa, na Ochaka.

Lindey Weey, Anita Bakari, na Brenda Achieng’ watadhibiti eneo la kati, huku Nasipwondi, Imbachi, na Ogola wataongoza safu ya mashambulizi.

Nahodha wa Uganda, Agnes Nabukenya ni tishio kuu, akiwa amefunga mabao sita katika raundi ya kwanza katika ushindi wa jumla wa 18-0 dhidi ya Nambia mwezi jana lakini akashindwa kufunga dhidi ya Kenya.

Uganda inayonolewa na kocha Sherly Botes kutoka Afrika Kusini walipangwa kufanya mazoezi yao ya mwisho Nyayo Jumamosi jioni.

Ili kuibwaga Kenya, anahitaji kuboresha safi ya mabeki na washambuliaji ambao hawakumakinika dhidi ya Kenya.
Junior Starlets wanahitaji sare au kuepuka kufungwa kwa zaidi ya magoli matatu ili kufuzu kwa raundi ya mwisho. Mshindi wa jumla atakutana na Cameroon katika raundi ya mwisho mwezi ujao baada ya timu hiyo kuzoa ushindi wa jumla wa 6-2 dhidi ya Ethiopia.
Kenya ilipewa tiketi ya kufuzu moja kwa moja pamoja na Zambia na Nigeria, ambazo zilikuwa zimeshiriki katika Kombe la Dunia la mwaka jana. Burundi, iliyo nafasi ya juu zaidi, pia ilifuzu kwa raundi ya pili.