Habari za Kitaifa

Kositany aonya kuhusu uhaba wa marubani wenye ustadi mpana

Na STANLEY NGOTHO November 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Serikali imeonya kuhusu upungufu unaonukua  wa marubani wenye ujuzi mpana wa anga unaozidi ustadi wa kuendesha ndege pekee, na sasa inataka mbinu jumuishi ili kuziba pengo hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (KAA), Caleb Kositany, anasema mabadiliko ya sekta ya usafiri wa anga duniani yanaendelea yanawanyima marubani wengi Wakenya fursa pana za ajira.

Bw Koisitany anasisitiza kuwa shirika hilo linalodhibiti masuala ya anga linasukuma mbinu jumuishi kukabili uhaba wa marubani ambao aliutaja kuwa janga la kimataifa.

“Taifa linakabiliwa na upungufu wa marubani wenye ujuzi mpana wa anga unaohitajika zaidi ya kuendesha ndege. Sekta ya anga inapanuka kila siku na ushindani ni mkali. Tuko kwenye mkondo mwafaka kama nchi katika kuwaandaa vijana wanaopenda masuala ya anga,” alisema Koisitany.

“KAA inasukuma mbinu jumuishi kuimarisha shule za mafunzo ya uchukuzi wa anga. Uwanja wa ndege wa Wilson unasalia kuwa wenye shughuli nyingi zaidi barani Afrika na asilimia 30 ya shughuli zake ni shule za mafunzo ya anga.”

Alikuwa akizungumza Jumatatu katika makao makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (KCAA) jijini Nairobi wakati wa hafla ya kutia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Chuo Kikuu cha Eastern Africa Baraton na Kenya School of Flying, kwa ajili ya kuanzisha Shahada ya Sayansi (BSc) ya Usimamizi wa Anga kwa marubani.

“Shahada ya usimamizi wa anga itawapa marubani wa Kenya nafasi bora katika soko la kimataifa, kando na leseni za kuendesha ndege ambazo shule nyingi zimekuwa zikitoa,” aliongeza Kositany.

Ukosefu wa ujuzi mpana wa anga unaozidi uwezo wa kuendesha ndege ni moja ya changamoto zinazodidimiza ushindani wa ajira kimataifa.

Kapteni Joseph Martin Ririani, mwanzilishi wa Kenya School of Flying na taasisi ya kwanza ya mafunzo ya marubani weusi nchini, alisema marubani wengi wa Kenya wanalazimika kusomea shahada zisizohusiana na anga ili kutimiza viwango vya kimataifa vya soko la ajira.

Alisema kuanzishwa kwa shahada hiyo kutawapa marubani ujuzi wa kutosha unaowawezesha kushiriki katika masuala ya biashara ya safari za ndege na ujasiriamali.

“Marubani wa Kenya hawatalazimika tena kusafiri hadi Amerika kusomea shahada za anga ambazo zimekuwa zikigharimu rasilmali nyingi na kuwa kikwazo kwa wengi. Marubani hawapaswi kuwa na mamlaka wakiwa angani tu, bali pia katika vyumba vya mikutano,” alisema Kapteni Ririani akionyesha matumaini kuwa kozi hiyo italeta mageuzi makubwa katika sekta ya anga.

Wanafunzi wanaosomea kozi ya urubani walisema kupatikana kwa shahada husika ndani ya nchi kutafanya elimu yao kupatikana kwa gharama nafuu na kuwarahisishia muda wa masomo.

Kozi hiyo, inayohusisha pia na mafunzo ya lugha za kigeni kwa marubani, itachukua miaka minne na marubani watakaohitimu watapatiwa leseni zitakazowezesha kushindania ajira duniani kote.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo wa Chuo Kikuu cha Eastern Africa Baraton, Dkt Paul Wahonya, alisema taasisi hiyo imebaini pengo lililopo katika mafunzo ya marubani na ushirikiano huo umeundwa kuliziba.

Kozi hiyo pia itahusisha mafunzo ya usimamizi wa fedha na masomo mengine yanayohusiana na anga, na marubani wanaohitimu watapatiwa leseni zitakazowawezesha kushindana kimataifa.