Uncategorized

Maandamano ya GenZ: Waziri Mkuu wa Bangladesha aliyeng’olewa mamlakani ahukumiwa kifo

Na REUTERS Na CHARLES WASONGA November 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI Mkuu  Bangladesh aliyetimuliwa mamlakani Sheikh Hasina Jumatatu, Novemba 17, alihukumiwa kifo baada ya kupatikana na kosa la kutekeleza uhalifu wa kibinadamu serikali yake ilipopambana na waandamanaji mwaka jana na kuchangia kutimuliwa kwake.

Waandamanaji hao walikuwa wanafunzi wa vyuo vikuu walioukuwa wakilalamikia ukosefu wa ajira, ubaguzi na kupanda kwa gharama ya maisha.

Watu wa familia za waathiriwa wa ghasia hizo waliokuwa wamefurika mahakamani walishangilia kwa furaha wakati majaji walikuwa wakisoma hukumu yao.

“Sheikh Hasina alitenda uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuchochea fujo, amri zake na kufeli kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa wa usalama waliotekeleza ukatili dhidi ya waandamanaji,” Jaji mmoja akasema alipotoa uamuzi wake.

“Ni wazi kwamba aliwachochea wanaharakati wa chama chake na kwamba aliamuru kuuawa kwa wanafunzi waliokuwa wakifanya maandamano,” Jaji huyo akaeleza.

Kile kilichoanza kama maandamano ya amani kuhusu ubaguzi katika uajiri wa watumishi wa umma kiligeuka kuwa shinikizo za kitaifa za kimtaka Hasina ajiuzulu.

Kilele cha machafuko hayo kilikuwa kuuawa kwa zaidi ya watu 1, 400, kulingana na Afisi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki.

Aidha, mahakama iliambiwa kuwa zaidi ya watu 25, 000 walijeruhiwa katika machafuko hayo.

Hasina alikabiliwa na mashtaka matano, yaliyohusiana na mauaji ya waandamanaji, kuagiza kunyongwa kwa baadhi yao, kuamuru matumizi ya silaha hatari pamoja na droni na helikopta kudumaza maandamano hayo.

Alikana mashtaka hayo.

Waziri huyo Mkuu wa zamani aliongoza Bangladesha kuanzia mwaka wa 2009 hadi 2024 alipong’olewa mamlakani.

Inahofiwa kuwa uamuzi wa mahakama uliotolewa jana huenda ukachangia kutokea kwa ghasia za kisiasa kuelekea uchaguzi wa kitaifa Februari 2026.