Mvutano mpya wa ardhi ya Kibiko afisa akidai hatimiliki feki zimetayarishwa
Mvutano mpya umeibuka kati ya serikali ya Kaunti ya Kajiado na Wizara ya Ardhi kufuatia madai ya kugawanya kimagendo na kutayarisha hati miliki ghushi za ardhi ya Kibiko, ambayo imesajiliwa kwa niaba ya jamii ya Iikeekonyokie katika Tarafa ya Kajiado Magharibi.
Kwa zaidi ya miaka saba iliyopita, ardhi hiyo ya thamani inayokadiriwa kufikia Sh100 bilioni imekuwa kiini cha migogoro ya uongozi, huku makundi mawili pinzani yakizozana vikali. Kundi moja linaongozwa na mwenyekiti wa muda mrefu Moses Parantai, naye mpinzani wake akiwa Moses Monik.
Mnamo Julai 2025, Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Kajiado ilimwamuru Moses Parantai kuwasilisha hati halisi ya umiliki wa ardhi ya Kibiko mahakamani ndani ya saa 72. Aidha, Jaji L Komingoi alielekeza kuwa iwapo Parantai atashindwa kutekeleza agizo hilo, basi Msajili Mkuu wa Ardhi atoe na kusajili cheti cha muda cha umiliki kwa jina la Moses Maseko Monik na wenzake kwa ardhi yenye nambari ya usajili LR No. Ngong/Ngong 12418. Kundi la Parantai lilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Hata hivyo, Waziri wa Kaunti anayesimamia Ardhi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Hamilton Parseina, alijitokeza hadharani akitoa madai mazito ya njama ya kughushi hati hizo. Alitaja mchakato huo kuwa wa udanganyifu uliowezeshwa na maafisa wa serikali, huku akilaumu mahakama kuwa sehemu ya “mfumo wa ufisadi unaoshamiri katika sekta ya ardhi.”
“Wanaohusika ni maafisa wa serikali walioko Ardhi House. Hati hizo feki zimetayarishwa katika kituo cha utoaji hati cha Ruaraka na sasa zinatayarishwa kupelekwa Ardhi House kutolewa kwa wanaolengwa wengi wao wakiwa watu wasio wenyeji na kampuni za binafsi,” alisema Parseina.
Katika kikao na wanahabari mjini Kajiado siku ya Alhamisi, Parseina alidai kuwa utayarishaji wa hati hizo ulianza Agosti 28 2025 na kukamilika Septemba 15 2025. Hata hivyo, hati hizo ziliwekwa tarehe Julai 14 2025 — siku mbili kabla ya Mahakama ya Rufaa kutoa agizo lake mnamo Julai 16 2025 hatua aliyosema ni sehemu ya njama ya kuharibu mchakato wa haki.
“Serikali ya kaunti haijawahi kutoa kibali chochote cha kugawa ardhi kupitia fomu ya PP2, wala hakuna fomu ya PPS1 iliyowasilishwa kwetu. Huu ni mchakato usiofuata sheria,” aliongeza.
Parseina alidai kuwa aliwaarifu maafisa wa juu kuhusu njama hiyo, akiwemo Waziri wa Ardhi Alice Wahome, kupitia ujumbe wa maandishi mnamo Agosti 28 2025 – siku ambayo mchakato huo wa kughushi ulitekelezwa lakini hakupewa majibu hadi leo.
“Ni jambo la kutisha kuona jinsi maagizo ya mahakama yanavyopuuzwa waziwazi na maafisa wa serikali. Wanasiasa pia wanahusika – wakiwemo maseneta na wabunge walioko madarakani. Wanashinikiza njama hii kwa maslahi yao binafsi. Hivi karibuni tutawataja hadharani,” Parseina alionya.
Kabla ya sakata ya Kibiko, Parseina alieleza kuwa kumekuwa na misururu ya unyakuzi wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo msitu wa Ololua, eneo la “400 Yard” katika milima ya Ngong, ardhi ya taasisi ya mifugo ya Ngong, na mashamba ya jamii za Torosei, Olodonyonyokie, Rombo, Mailua, Mbirikani na Kuku.
“Kuna afisa mmoja wa ngazi ya juu katika Ardhi House ambaye ameonekana kuhusika katika njama hizi zote. Ikiwa hali hii itaendelea, ninasema wazi – kutakuwa na vurugu kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi, na hatimaye hati miliki zitapoteza maana na thamani hapa Kajiado,” alionya.
Parseina alitoa wito kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kufanya uchunguzi wa kina kuhusu biashara hiyo chafu katika ofisi ya ardhi na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika.