Polisi watibua njama ya vijana waliokodisha chumba kwa sherehe ya ngono
POLISI mjini Kisii wamewakamata vijana 23 wanaoshukiwa kupanga sherehe ya ngono.
Wanane kati ya vijana hao ni wa umri chini ya miaka 18 ilhali 15 wametimiza miaka 18 na kuendelea.
Kulingana na ripoti ya polisi, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutoka Kaunti Ndogo ya Kitutu ya Kati walipata habari kwamba baadhi ya vijana walikuwa wamekodi chumba katika eneobunge la Nyanchwa, viungani mwa mji wa Kisii na kuwaalika marafiki zao kwa vinywaji vya bure na ngono isiyo na kikomo Jumatano jioni.
“Maafisa wa DCI kutoka Kaunti Ndogo ya Kitutu ya Kati wakati walipata habari za kijasusi kuhusu waliyopanga vijana hao na walivamia jumba la vyumba vya kukodisha Matano Nyanchwa. Walifanikiwa kuwakamata watu 23 hasa watoto waliokuwa wamekodi chumba kwa shughuli zinazoshukiwa kuwa haramu. Kulingana na taarifa iliyotolewa ni kwamba vijana hao walikuwa wamealika wenzao kwa vinywaji na ngono katika ghorofa hiyo,” ilisoma sehemu ya ripoti hiyo ya polisi.
Baada ya kupekua chumba hicho, maafisa hao walipata vileo vya pombe ya makali, pakiti za sigara na kondomu kadhaa.
Washukiwa hao walisindikizwa hadi Kituo cha Polisi cha Nyanchwa na wazazi wao kujulishwa kuhusu kukamatwa kwao.
Tukio hilo linafanana na lingine lililotokea miaka mitatu iliyopita katika eneo la Mwembe, mita chache tu kutoka mtaani Nyanchwa.
Katika tukio hilo, polisi waliwakamata wanafunzi wanane kutoka shule mbili ambao pia walikuwa wamepanga kufanya ngono baada ya kutoroka shuleni mwao.
Waliokamatwa ni wanafunzi watatu kutoka Shule ya Nduru Girls na wavulana watano kutoka Shule ya Upili ya St Joseph’s Nyabigena.
Pia walikuwa wamepanga chumba kimoja ndani ya eneo hilo ili kujiburudisha.
Saba kati yao walikuwa watahiniwa wa KCSE.
Polisi walipowahoji kwa nini walikusanyika kwenye chumba hicho, walidai kuwa walitaka kupika chakula kisha kutawanyika hadi nyumbani kwao.
Msichana mmoja alifanikiwa kukwepa mtego huo wa polisi.
Waliokamatwa walipelekwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii kwa uchunguzi wa kimatibabu kufahamu iwapo walijihusisha na tendo la ndoa au la.