Uncategorized

Raila aelekea mataifa ya Kiarabu baada ya kupokewa vizuri Afrika Magharibi kampeni za AUC

Na JUSTUS OCHIENG’ December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga sasa anaelekeza kampeni zake katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika kutafuta kura za uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) baada ya kampeni yake kufana Afrika Magharibi.

Eneo la Kaskazini mwa Afrika linashirikisha mataifa ya Morocco, Algeria, Tunisia, Libya na Mauritania.

Mwenyekiti mwenza wa sekritariati ya kuongoza kampeni za Bw Odinga, Balozi wa zamani wa Kenya nchini Amerika, Elkana Odembo, alisema kuwa kiongozi huyo ataondoka nchini leo kuelekea eneo hilo maarufu kama “Maghreb”.

“Eneo ambako tunalenga sasa na lile la Kaskazini mwa Afrika, maarufu kama ‘Maghreb’. Baada ya hapo tutajiandaa kwa mjadala wa umma (Mjadala Afrika) mnamo Desemba 13, 2024,” Bw Odembo akaeleza.

Pendekezo kuhusu Kamati ya Wawakilishi

Mnamo Machi mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Afrika (AU) liliidhinisha pendekezo la Kamati yake ya Wawakilishi (PRC) kwamba  eneo la Mashariki mwa Afrika ndilo litoe wawaniaji wa wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Nalo eneo la Kaskazini mwa Afrika lilipewa nafasi ya kuteua wawaniaji wa wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa AUC.

Bw Odinga anapambana na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard James Randriamandrato na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Mauritius Anil Kumarsingh Gayan.

Lakini uwaniaji wa Bw Gayan unaonekana kuwa utafeli baada ya Waziri Mkuu mpya wa Mauritius Navinchandra Ramgoolam kumhakikishia Rais William Ruto kuwa nchini yake inaunga mkono azma ya Bw Odinga.

Katika uchaguzi wa ujao utakaofanyika Februari 5, 2025, Afrika Kaskazini itatoa Naibu Mwenyekiti wa AUC.

Kinyang’anyiro cha naibu mwenyekiti kimevutia wawania sita ambao ni pamoja na; Francis Sala na Selma Malika kutoka Algeria, Mohamed Ahmed Fathi na Hanan Morsy kutoka Misri, Najat M. Elhajjaji kutoka Libya na Latifa Akharbach kutoka Morocco.

Wadadisi wanasema kampeni za Bw Odinga Kaskazini mwa Afrika itakumbukwa na changamoto kwani mataifa hayo yatamtaka aunge mkono wagombeaji wao kwa cheo cha naibu mwenyekiti.

Wataweka maono yao kwenye Mdahalo

Hatua hiyo huenda ikakasirisha wawaniaji wengine na mataifa yao.

Bw Odinga anatarajiwa kukabiliana na wapinzani wake kwa kiti hicho katika Mjadala Afrika mnamo Desemba 13 ambako wataweka wazi maono na mipango yao katika kutekeleza Ajenda ya Afrika ya 2063.

Mjadala huo utapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga katika mataifa yote ya Afrika.

Bw Odinga anasema kuwa yeye ndiye mwaniaji bora akieleza kuwa maoni yake ni kuhakikisha kuwa amani, utangamano na ushirikiano unafikiwa Afrika.

Tume ya Umoja wa Afrika ilisema kuwa “Mjadala Afrika” utatoa nafasi kwa wawaniaji wote kuelezea kwa kina mipango yao ya kuboresha bara hili.

Mjadala huo ambao utafanyika katika makao makuu ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia utaendeshwa kwa lugha za Kifaransa na Kiingereza.

Tafsiri za mjadala huo zitatolewa kwa wawaniaji na raia wa nchini za Afrika, kwa lugha sita za Umoja wa Afrika ambazo ni; Kiingereza, Kifaransa, Kiarabu, Kireno, Kihispania na Kiswahili.