Ramadhani yaanza Wakenya wakilia msoto kutokana na hali ngumu
BAADHI ya waumini wa Kiislamu nchini wameanza mwezi mtukufu wa Ramadhani wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha ambayo inakisiwa itafanya msimu huo kuwa mgumu zaidi.
Kuongezeka kwa bei ya vyakula huenda kukaathiri uwezo wao wa kupyata mlo unaostahili wa mfungo.
Katika soko la Marikiti, Kaunti ya Mombasa, waumini walikuwa wakijitayarisha kwa msimu ila wanakabiliwa na wakati mgumu wa kifedha wakisubiri misaada.
“Katika miaka ya hivi karibuni Ramadhani imekuwa tofauti kutokana na hali ngumu ya kiuchumi. Nilikuwa nikinunua chakula kwa wingi kabla ya Ramadhani, lakini mwaka huu naweza tu kununua kile familia yangu inahitaji kwa siku, na wakati mwingine hata kidogo zaidi,” akasema Bi Amina Mussa mkazi wa Mombasa.
Wengi wanalalamikia kupanda kwa bei za vyakula hasa tende ambayo ni muhimu kwa futari.
“Sasa tunanunua tende Sh200 kwa pakiti au debe ilhali hapo awali ziligharimu kati ya Sh50-100,” alisema Mawazo Omar ambaye ni mchuuzi katika soko hilo.
Ili kupunguza mzigo huu kwa familia zisizojiweza misikiti, makanisa, mashirika ya misaada na wahisani wamejitokeza kusaidia kwa kusambaza chakula na kuandaa futari za bure.
Mashirika kama New Life Prayer Center, Jawn Community Trust na Jaffer Foundation yameanzisha mipango ya kugawa chakula ili kuhakikisha familia hazilali njaa wakati huu wa mwezi mtukufu.
“Ramadhani ni mwezi wa kutoa na tunahimizwa kuwasaidia wale wanaohitaji. Wengi wanapitia ugumu mkubwa kipindi hiki na tunaomba wafadhili wa Kiislamu waendelee kutoa kwa ukarimu, lakini wafanye hivyo kwa tahadhari,” akasema Mohammed Ismael mwenyekiti wa Jawn Community.
Harakati za kutoa misada hazijaishia kwa Waislamu pekee.
Katika jamii nyingi, mashirika ya Kikristo na watu binafsi pia wanashiriki kwa kuwapa maskini na wasiojiweza chakula na misaada.
“Kuwajali maskini ni jukumu la waumini wa dini zote,” alihoji mhubiri Ezekiel Odero wa kanisa la New Life.
“Ramadhani ni wakati wa kutoa, na inatia moyo kuona watu wa imani tofauti wakija pamoja kusaidia wenye mahitaji,” akaongeza.
Wakati huo huo, Ramadhani ya mwaka huu imeanza kwa tofauti huku baadhi ya Waislamu wakianza kufunga tarehe tofauti kutokana na utofauti wa mbinu za kuona mwezi.
Wengine walianza kufunga jana huku wengine wataanza leo wakifuata mamlaka na mapokeo tofauti ya kidini.