Safari ya Maasai Mara iliyokatiza maisha ya watalii 10 na rubani
SAFARI ya watalii kuelekea Maasai Mara ilikatizwa ghafla jana asubuhi baada ya ndege ndogo ya kampuni ya Mombasa Air Safari, iliyokuwa imebeba abiria 11 akiwemo rubani, kuanguka katika msitu wa Nyando, eneo la Matuga, Kaunti ya Kwale, na kulipuka moto.
Ndege hiyo aina ya Caravan, yenye nambari za usajili 5Y-CCA, iliondoka Uwanja wa Ndege wa Diani saa mbili na dakika ishirini na tano asubuhi, ikielekea Kambi ya Kichwa Tembo katika Hifadhi ya Maasai Mara, Kaunti ya Narok. Kambi hiyo ya kifahari ni maarufu kwa mandhari yake mazuri na ukaribu wake na njia za uhamaji wa nyumbu.
Abiria waliokuwa wamepanga mapumziko ya kifahari walikuwa ni watalii wanane kutoka Hungary, wawili kutoka Ujerumani, na rubani mmoja Mkenya. Kwa masikitiko, wote waliangamia.
Walioshuhudia walisema ajali hiyo ilitokea mvua kubwa ilipokuwa ikinyesha na kusababisha ukungu mzito uliopunguza mwonekano. Bw Hamadi Garashi, mkazi wa eneo hilo, alisema waliposikia mlipuko mkubwa, walikimbia eneo la tukio na kukuta moto mkubwa ukiwaka.
“Tuliposikia mlipuko, tulikimbia tukadhani ni radi. Tulipofika, tuliona moto mkubwa na mabaki ya ndege. Tulimjulisha afisa wa kijiji ambaye aliarifu maafisa wengine wa serikali,” alisema Bw Garashi.
Mkazi mwingine, Bw Makopa Sazu, alisema hali ya hewa ilikuwa mbaya kiasi kwamba ilikuwa vigumu hata kuona ardhini.
“Niliposikia mlio, nilikimbia na kufika eneo la ajali. Nilikuta moto mkubwa na sehemu za miili zikiwa zimezagaa,” alisema.
Mvua kubwa ilitatiza juhudi za uokoaji katika kijiji cha Nyando, huku magari ya dharura yakitatizika kufika eneo la ajali kutokana na matope na miinuko eneo hilo.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (KCAA) kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Emile Arao,ilithibitisha ajali hiyo, ikisema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo chake.

Waziri wa Uchukuzi, Davis Chirchir, alisema ndege hiyo ilipoteza mawasiliano ya rada na mnara wa udhibiti wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mombasa muda mfupi kabla ya kuanguka.
“Wote waliokuwa kwenye ndege walipoteza maisha. Idara ya Uchunguzi wa Ajali za Ndege (AAID) imetumwa eneo la tukio kufanya uchunguzi wa kina,” alisema Waziri.
Mwenyekiti wa Mombasa Air Safari, Bw John Cleave, alithibitisha kuwa ndege hiyo ilikuwa safarini kuelekea Maasai Mara, na kwamba hakuna aliyenusurika. Aliongeza kuwa kampuni hiyo imeunda kikosi kutoa ushauri na kuratibu shughuli za mazishi.
Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, alituma rambirambi kwa familia za marehemu na kuwaonya madereva kuwa waangalifu wakati huu wa mvua kubwa.
Ajali hiyo ilijiri saa chache baada ya watu watano kufariki Jumatatu usiku katika ajali ya barabarani iliyotokea mjini Keroka, mpakani mwa kaunti za Kisii na Nyamira.
Ajali hiyo ilihusisha trela lililokuwa lilitoka Nyangusu na waendeshaji wa pikipiki.
Kulingana na kamanda wa trafiki wa Masaba Kaskazini Peter Chege, dereva wa trela hiyo anasemekana kukosa kulidhibiti lilipokuwa likiteremka sehemu ya barabara ya Ichuni-Keroka.
Baada ya lori hilo kukosa mwelekeo, lilibingiria barabarani na kuwaangukia wanabodaboda watatu walikuwa kando kando mwa barabara wakingoja wateja katika solo Hilo.
Mkuu huyo wa trafiki aliongeza kuwa dereva wa trela hiyo naye pia alipoteza maisha yake na mtu mwingine aliyekuwa naye humo ndani.
“Inashukiwa kuwa dereva wa trela alishindwa kulidhibiti. Lakini tumeanzisha uchunguzi kujua ni nini kilienda vibaya,” Bw Chege aliwambia Taifa Leo kwa simu.
Afisa huyo wa polisi aliwataka madereva wa magari kuwa waangalifu wanapoteremka sehemu hiyo ya barabara kwa kuwa ina sifa mbaya ya kusababisha ajali.
“Eneo hilo ni hatari. Tunawaomba madereva kuwa waangalifu kila wanapofika eneo hilo haswa wakati huu ambapo tunashuhudia mvua kubwa,” Bw Chege alisema.
Ajali ya Keroka iliongeza idadi ya ajali za barabarani zilizoshuhudiwa kote nchini wiki hii, ambapo ripoti zinaonyesha kuwa watu 17 wamepoteza maisha katika kipindi cha saa 72