Habari

Uwekezaji mpya sasa kufagia mbali kilimo cha mkonge Pwani

Na ANTHONY KITIMO October 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI ya mashamba ya Rea Vipingo, ambayo ilikuwa nguzo kuu ya sekta ya mkonge nchini Kenya, sasa imeanza mchakato mkubwa wa kubadili matumizi ya ardhi kutoka kilimo hadi uwekezaji wa mali isiyohamishika na maendeleo ya viwanda.

Mashamba makubwa ya mkonge yaliyokuwa yakitawala uchumi wa Pwani kwa miongo kadhaa, sasa yanageuzwa kuwa maeneo ya makazi ya kifahari, viwanja vya gofu, nyumba za kifahari na viwanda.

Hatua hii imechochewa na kushuka kwa mapato ya mkonge na ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa matumizi ya kibiashara na kiuchumi.

Katika taarifa ya mwaka 2024, kampuni ya Rea Vipingo ilifichua kuwa tayari imekabidhi ekari nyingi za mashamba ya mkonge kwa kampuni ya Centum Investment, baada ya makubaliano yaliyoafikiwa mwaka 2015.

Centum sasa inasimamia mradi mkubwa wa maendeleo ujulikanao kama Vipingo Special Economic Zone (VSEZ).

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Centum Vipingo, Bw Martin Kariuki, zaidi ya ekari 10,254 za mashamba ya mkonge sasa zinageuzwa kuwa maeneo ya uwekezaji katika sekta mbalimbali.

“Tuna maeneo yaliyotayarishwa kwa ujenzi wa nyumba, viwanda, biashara na hata taasisi za elimu na afya.

Pia tumewekeza katika miundombinu muhimu kama mtambo wa kusafisha maji ya bahari wenye uwezo wa lita milioni 3 kwa siku na kituo cha umeme” alisema Bw. Kariuki.

Katika ripoti yake, Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) ilieleza kuwa uzalishaji wa mkonge nchini umepungua kutoka tani 14,806 mwaka 2022 hadi tani 11,432 mwaka 2023.

Hali hii imezua taharuki miongoni mwa wakulima, hasa kutokana na kushuka kwa bei ya mkonge katika soko la kimataifa.

Kwa sasa, mradi wa VSEZ unatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 200 vitakavyohusika katika usindikaji wa mazao, utengenezaji wa bidhaa, teknolojia, nishati safi, dawa na huduma za usafirishaji.

Mradi huu unatarajiwa kutoa ajira zipatazo 50,000 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.Rais William Ruto alisema mradi huu ni kielelezo halisi cha uwezo wa ugatuzi katika kuleta maendeleo ya kweli na kuongeza fursa za ajira.

Gavana wa Kilifi, Gideon Mung’aro, asema kuwa ongezeko la uwekezaji katika eneo la Vipingo limeongeza thamani ya ardhi na kuvutia kampuni nyingi kuwekeza katika eneo hilo, hasa kutokana na mpango wa kupanua barabara ya Mombasa-Kilifi.

Katika kaunti jirani ya Taita-Taveta, kampuni ya Teita Sisal Estate Limited pia imetangaza mpango wa kugawanya na kuuza ekari 3,000 za ardhi kwa wawekezaji binafsi kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa mkonge.