Uncategorized

Wanga ajitetea kwa kujenga mochari

Na GEORGE ODIWUOR November 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Homa Bay, Gladys Wanga, ametetea uamuzi wake wa kukamilisha ujenzi na kufungua rasmi chumba kipya cha kuhifadhia maiti, licha ya mradi wa ujenzi wa kituo cha dharura na ajali katika hospitali kuu ya rufaa ya kaunti hiyo kuchelewa kukamilika.

Bi Wanga alisema chumba cha kuhifadhia maiti ni huduma muhimu kama vile majengo mapya ya hospitali yanayoendelea kujengwa.

Alisisitiza kuwa sekta ya afya ina maeneo kadhaa nyeti, na huduma za mochari ni miongoni mwao.

Chumba hicho kipya cha kuhifadhia maiti, ambacho kilifunguliwa rasmi Alhamisi, kina uwezo wa kuhifadhi miili 137, ikiwemo 37 katika sehemu ya watu binafsi.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi na watumiaji wa mitandao ya kijamii wameikosoa serikali ya kaunti hiyo, wakidai kuwa gavana anaweka kipaumbele katika miradi isiyo ya dharura.

Wamehoji kwa nini ujenzi wa jengo la hospitali lenye thamani ya Sh200 milioni, ulioanza Machi 2023, haujakamilika, ilhali makao makuu mapya ya kaunti yalimalizika kwa muda mfupi na kufunguliwa na Rais William Ruto mwezi Agosti mwaka huu.

Miongoni mwa wakosoaji wakuu wa Bi Wanga ni Odoyo Owidi, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Maendeleo ya Maji Kusini mwa Ziwa Victoria. Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Bw Owidi alisema ujenzi wa ofisi si kipaumbele, akitaja mradi huo kama “anasa.”

Lakini Bi Wanga alitetea utendakazi wake, akisema serikali yake imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya, ikiwemo kuinua hospitali ya rufaa ya Homa Bay kutoka Level 4 hadi Level 5.

“Tulipoingia ofisini mwaka 2022 hospitali ilikuwa ya ngazi ya nne. Kupitia juhudi zetu na msaada wa Wizara ya Afya, tumeweza kuinua huduma na sasa wananchi wanapata matibabu bora,” alisema Bi Wanga.

Aliongeza kuwa wakati wa kampeni, wakazi walimwomba kujenga mochari mpya kwa sababu ile ya zamani, iliyojengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi maiti 20 pekee na mara nyingi ilikuwa imejaa.

“Wakati mwingine mwili wa marehemu ulilazimika kuwekwa juu ya mwingine. Watu wengi walikuwa wanalazimika kupeleka wapendwa wao kwenye mochari za kibinafsi,” alisema.

Bi Wanga alisema lengo la ujenzi huo ni kuhakikisha watu wote wanapata mazishi yenye heshima. “Wote tutafika mwisho wa safari ya maisha. Ni muhimu tuwape wafu wetu heshima wanazostahili,” aliongeza.

Mbali na kuhifadhi miili, alisema mochari hiyo itatumika pia na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Matibabu Kenya (KMTC) wanaosomea taaluma ya huduma za mochari.