Uncategorized

Wazazi wa wanafunzi wa shule za bweni kulipa karo sawa kuanzia mwaka ujao

Na MERCY SIMIYU, WINNIE ATIENO November 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZAZI wa wanafunzi wanaojiunga na shule za upili za bweni kuanzia Januari 2026 wamepata mshtuko baada ya Wizara ya Elimu kutangaza mwongozo mpya wa kujiunga na shule za upili chini ya mtaala unaotegemea umilisi (CBC).

Mwongozo huo unasema kuwa wanafunzi wote wa shule za bweni watatakiwa kulipa karo sawa ya shule bila kujali shule watakayochaguliwa kusomea.

Aidha, mwongozo huo umepunguza kiasi cha fedha kinachotengwa kwa shule za kutwa (FDSE), kwani wanafunzi wa watalipa sehemu ya karo ya shule. Kwa wakati huu, wazazi wanalipa karo kulingana na aina ya shule (kitaifa, mkoa au za kaunti) ili kupunguza mzigo wa kifedha.

Kulingana na mwongozo huo, karo ya shule za bweni itabakia Sh53,554 kwa mwaka. Wazazi wa wanafunzi wa shule za kutwa watalipa Sh9,374, na wanafunzi wenye mahitaji maalum watalipa Sh37,210. Serikali itatoa mgao wa Sh12,870 kwa kila mwanafunzi wa shule za kutwa na Sh32,600 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mwongozo huo unalenga kusawazisha karo katika shule za bweni na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma kutokana na hali ya kifedha. Pia unafafanua mipaka ya umri na madarasa, huku shule za upili zikihudumia wanafunzi wa miaka 15–17 (gredi 10–12) na kuunda daraja kati ya shule za msingi na elimu ya juu.

Shule zote lazima ziwe na miundombinu ya kisasa, ikijumuisha maabara, studio za sanaa, uwanja wa michezo, warsha, na vyumba vya kidijitali. Kila darasa katika shule za  bweni halipaswi kuwa na zaidi ya wanafunzi 45.

Walimu watafundisha angalau masomo 27 kwa wiki, huku wakuu wa shule wakipunguziwa mzigo wa kufundisha ili kuzingatia uongozi.

Mpangilio wa masomo utafuata mfumo wa masomo 40 kwa wiki. Vipindi vya michezo vitakuwa 3 kwa wiki, ICT 2, na somo la kujifunza 1. Shule za kutwa hazitawalazimisha wanafunzi kufika mapema kabla ya saa moja na robo asubuhi, na masomo yatamalizika tisa na nusu jioni.

Shule zinapaswa pia kuunda kamati za ukaguzi wa fedha, huku wazazi na viranja wa wanafunzi wakishirikishwa katika utawala.