Habari

Upasuaji waonyesha Sharon Otieno alidungwa kisu mara 8

September 7th, 2018 2 min read

Na RUTH MBULA

RIPOTI ya Daktari Mkuu wa Upasuaji Maiti wa Serikali, Johansen Oduor ilionyesha kuwa Sharon Otieno alidungwa kisu mara nane kabla ya mwili wake kutupwa kichakani.

Dkt Oduor alisema mwanafunzi huyo alikufa baada ya kuvuja damu kutokana na majeraha mwilini.

“Ripoti ya upasuaji imeonyesha kuwa alidungwa mara tatu nyuma ya shingo, mara nne mgongoni na mara moja kushoto mwa tumbo lake,”alisema Dkt Oduor.

Vile vile, daktari alisema marehemu alikuwa na alama za kunyongwa shingoni.

Kulingana na ripoti hiyo, Sharon alikuwa na majeraha mengi, ishara kwamba aling’ang’ana na wauaji wake kabla kufariki.

Mwanafunzi huyo wa chuoni alidungwa tumboni kutoka nyuma, na mtoto aliyekuwa naye tumboni alifariki kutokana na jeraha hilo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Vile vile, kuna uwezakano kwamba alibakwa. Dkt Oduor aliambia Taifa Leo kuwa, sampuli kadha zitapelekwa katika maabara ya serikali kwa uchunguzi.

Maelezo zaidi yaliibuka jana jinsi Sharon alivyouawa kinyama na mwili wake uliokuwa na kijusi cha miezi saba kutupwa kichakani.

Maafisa wa ujasusi waliokagua mwili wa Sharon walidokezea Taifa Leo kuwa mwili wake ulikuwa na majeraha mabaya ya kudungwa na kisu mgongoni, shingoni na mikononi.

Aidha, inahofiwa kuwa kisu kilichotumika kumdunga kiliacha shimo katika tumbo lake la uzazi.

Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Rongo alikuwa na mimba ya miezi saba.

Baadhi ya jamaa na familia yake waliambia Taifa Leo kuwa, mwili wake mwanafunzi huyo ulikuwa na alama nyingi za kisu kudhihirisha kuwa alidungwa mara kadhaa katika maeneo mengi mwilini.

Maafisa wa upelelezi waliotumwa kutoka Nairobi kwenda kufanya uchunguzi waliambia wanahabari jana kuwa, walishtushwa na hali waliyokumbana nayo eneo ambao mwili ulipatikana.

“Sijashuhudia kamwe hali kama hii. Inatisha,” akasema mmoja wa makachero hao ambaye hakutaka kutambulika.

Vile vile, walisema mwanafunzi huyo yawezekana alibakwa kabla kuuawa kinyama kwani mipira kadhaa ya kondomu iliyokuwa imetumika ilipatikana karibu na pahali ambapo mwili ulikuwa umetupwa.

Baada ya kuzuru eneo hilo, polisi pia walisema eneo mwili huo ulipatikana kulikuwa na damu nyingi.

Mwili wa Sharon ulipatikana umetupwa karibu na msitu wa Kopedo, Kaunti ya Homa Bay, siku mbili baada ya mwanadada huyo kutoweka.

Mara ya mwisho alionekana katika hoteli moja Kaunti ya Migori alikokuwa amepanga kukutana na mwandishi wa gazeti la Nation, Bw Barack Oduor.

Kulingana na mwandishi huyo, walitekwa nyaraka Jumatatu jioni lakini alifanikiwa kutoroka aliporuka nje ya gari walilokuwa wamebebwa ndani.

Polisi jana walisema wanawasaka washukiwa wanne waliohusika na utekaji nyara huo.

Sampuli za DNA zimechukuliwa kutoka kwa mshukiwa mkuu Michael Oyamo, msaidizi wa Gavana wa Migori Okoth Obado, ambaye amehusishwa pakubwa na kisa hicho.

Hayo yakijiri, shangazi wa marehemu anasemekana ‘kuaga dunia kutokana na mshtuko’ alioupata baada ya kupokea habari za kifo cha Bi Otieno.

Msemaji wa familia Joshua Okongo alisema Bi Deborah Ogweno, 44, alizirai Jumatano na “kisha kufariki” Ijumaa asubuhi.

Wakati huo huo, uchunguzi wa maiti ya marehemu ulifanywa jana alasiri katika mochari ya hospitali ya Rachuonyo Level Four, Kaunti ya Homa Bay.

Jamaa zake wa karibu, makachero na Daktari Mkuu wa Upasuaji Maiti wa Serikali, Dkt Johansen Oduor, walikuwa katika mochari hiyo.

Shughuli hiyo ya upasuaji maiti ilianza saa nane mchana.

Hisia kali zilichacha baada ya familia ya marehemu, miongoni mwao mamake, Melinda Auma, kuwasili katika hospitali hiyo muda mfupi kabla saa sita adhuhuri.

Wakili Cliff Ombeta pia alikuwa katika mochari hiyo. Aliambia wanahabari kwamba anawakilisha Gavana wa Migori Okoth Obado.