Habari za Kaunti

Usafi wa Hoteli: Maafisa wa mazingira Nairobi motoni

Na WINNIE ONYANDO August 24th, 2024 1 min read

WIKI moja tu baada ya Afisa Mkuu wa Mazingira Kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria kufunga hoteli moja jijini kwa kukosa kudumisha viwango hitajika vya usafi, kamati ya Afya kaunti hiyo sasa inataka Mkurugenzi wa masuala ya Usafi na mazingira jijini Margaret Sunguti ahamishwe.

Akizungumza na Taifa Leo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Afya, Diwani Maurice Ochieng alisema kuwa Bi Sunguti anafaa kuhamishwa kwa sababu ameshindwa kufanya kazi.

“Kutokana na kile tulichoshuhudia siku chache zilizopita kuhusu uchafu mikahawani, kama kamati tumeamua kuwa Bi Sunguti ahamishwe haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Ochieng.

Kando na hayo, diwani huyo wa Mountain View alisema kuwa kamati hiyo inapendekeza Waziri wa Afya Susan Silantoi ahakikishe kuwa anamhamisha afisa anayesimamia Usalama wa Chakula, afisa anayesimamia masuala ya kupima chakula ili kujua ikiwa ni salama kwa matumizi ya umma katika kaunti na hilo linafaa kufanywa mara moja.

“Hii ni kwa sababu maisha ya watu wa Nairobi yako hatarini na hatuwezi kukaa kama kamati kusubiri kuona wengi wakienda hospitalini kwa sababu ya kula chakula kisicho salama kutokana na uzembe wa watu wengine,” akaongeza Bw Ochieng.

Kwa upande mwingine, kamati hiyo inamtaka afisa mkuu wa Afya ya Umma Tom Nyakaba kuwa thabiti na kuhakikisha anamhamisha afisa ambaye anasimamia kaunti ndogo ya Starehe ndani ya saa 48 kwa sababu wakazi wa Nairobi wanataka huduma bora.

Haya yanajiri siku saba tu baada ya Bw Mosiria kufunga mkahawa unaoandaa vyakula kama vile mayai, kebab na smokies ambavyo husambazwa kwa wachuuzi wa mitaani.

“Alikabidhiwa barua ya kufunga biashara. Unapowakamata na kuwafikisha mahakamani, wengi huachiliwa kwa dhamana.  Baada ya kulipa dhamana hiyo wanarejea kuendeleza biashara bila kujali usafi,” alisema Bw Mosiria.