Habari za Kitaifa

Usafirishaji wa vipande vyembamba vya miti nje ya nchi wapigwa marufuku

Na WYCLIFFE NYABERI August 27th, 2024 1 min read

SERIKALI imesitisha usafirishaji wa vipande vyembamba vya mbao, maarufu kama vineyeer, nje ya nchi.

Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi, na Misitu Aden Duale, alitangaza kusimamishwa kwa mauzo ya malighafi hayo mnamo Jumatatu, Agosti 27, 2024 na kuongeza kwamba uamuzi huo unafaa kuanza kutekelezwa mara moja.

Bw Duale aliamuru Shirika la Huduma za Misitu Nchini (KFS) kutotoa barua yoyote ya kupinga kusafirishwa kwa malighafi hayo nje ya nchi, akidokeza kuwa marufuku hiyo ni hatua madhubuti ya kuunga mkono mikakati ya Kitaifa wa kutunza mazingira.

Waziri Duale aidha aliongeza kuwa mikakati hiyo inalenga kurejesha hekta milioni 10.6 za mandhari iliyoharibiwa kwa kupanda miti bilioni 15 kama kielelezo cha dhamira isiyoyumba ya serikali ya kudumisha mazingira.

“Ripoti za hivi punde zimeangazia uvunaji wa mapema wa miti ambayo haijakomaa kwenye mashamba, jambo ambalo linatishia mafanikio ya juhudi za serikali za upandaji miti. Kwa kusitisha uuzaji wa nje wa malighafi hayo, serikali inakusudia kukomesha tabia hii, kuhakikisha miti inaruhusiwa kukomaa na kuchangia ipasavyo katika malengo ya urejesho wa kitaifa,” ilisema sehemu ya barua ya Waziri Duale.

Aliongeza, “Ahadi ya serikali ya kufikia asilimia 30 ya miti ifikapo mwaka 2032 haijayumba. Kusitisha usafirishaji huo ni muhimu ili kulinda mustakabali wa mazingira ya Kenya na inapaswa kuwatia moyo wadau wote kujiunga nasi katika jitihada hizi muhimu”.