Habari za Kitaifa

Wachuuzi wanne washtakiwa kuuza dawa ‘feki’ ya kuua mende

February 22nd, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WACHUUZI wanne wameshtakiwa kwa kuuzia wateja dawa ya kuua mende ambayo haijaidhinishwa na serikali.

Watson Mwangi Macharia, James Mwangi Njeri, Wanjiru Wainaina, na Alberta Barbra Odhiambo walikana mashtaka mawili ya kuuza dawa ya kuua mende na wadudu wengine wanaotambaa ambayo walijua haijakubaliwa kisheria.

Macharia, Mwangi, Wanjiru, na Barbra walikana shtaka mbele ya hakimu mwandamizi Bernard Ochoi kwamba walikuwa wanauza dawa hiyo ya kuua mende kabla haijasajiliwa na asasi inayohusika na serikali.

Wanne hao walikabiliwa na shtaka la kuuza dawa hiyo kinyume cha sheria za kudhibiti wadudu nambari 4(1).

Shtaka lilisema sheria hii ya kudhibiti dawa za kuua wadudu ilifanyiwa marekebisho mnamo 2009 kuruhusu asasi husika ya serikali isajili dawa zote za kuua wadudu ambazo Wakenya huuziwa.

Shtaka dhidi ya wanne hao lilisema mnamo Februari 16, 2024, katika mnara wa Tom Mboya kwenye barabara ya Tom Mboya walikamatwa na maafisa wa serikali kutoka kitengo cha kudhibiti dawa za sumu wakiuza dawa ya kuua mende na wadudu wengine kama “haijasajiliwa na asasi husika ya serikali.”

Watson alikabiliwa na shtaka peke yake la kupakia ndani ya gari lake dawa hiyo ya kuua wadudu bila idhini ya asasi husika ya kudhibiti.

Washtakiwa hao walikana shtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Hakimu aliorodhesha kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili kutengewa siku ya kusikilizwa.