Habari za Kitaifa

Wakenya watahadharishwa kuhusu kimbunga IALY

May 21st, 2024 2 min read

NA WACHIRA MWANGI 

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetoa tahadhari kwa wenye boti ndogo kusitisha shughuli zao baharini kutokana na athari za kimbunga IALY ambacho kimeongeza nguvu.

Onyo hili linatokana na utabiri unaoonyesha uwezekano wa mvua kubwa na hali mbaya ya bahari kuanzia Jumapili hii ambayo imepita, hali inayotarajiwa kuendelea hadi mwisho mwa wiki hii.

Kwa mujibu wa tahadhari hiyo, mvua inatarajiwa kuzidi milimita 30 kwa saa 24 katika maeneo mbalimbali, haswa eneo la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, na Nyanda za Juu zote za magharibi na mashariki mwa Bonde la Ufa, ikijumuisha eneo la jiji kuu la Nairobi.

Hata hivyo, wasiwasi mkubwa ulioangaziwa na idara hiyo ni hali mbaya ya baharini inayotarajiwa kuambatana na kimbunga hicho.

“Mvua kubwa inaweza kufikia zaidi ya milimita 40 kwa saa 24 katika maeneo haya, hasa kuanzia Mei 19 hadi Mei 24, 2024. Hata hivyo, mvua inatarajiwa kupungua kuanzia Jumatano lakini itaongezeka tena pwani na kuendelea hadi Ijumaa,” alisema Dkt David Gikungu, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa.

Mabaharia wameonywa kuwa mvua hiyo kubwa itakuwa ikifuatana na upepo mkali wa kusini, mawimbi makubwa ya bahari, na hali mbaya ya baharini.

“Kwa sababu ya Kimbunga IALY, tutarajie upepo mkali wa Kusi ambao huvuma Kusini-Mashariki. Kasi ya upepo huo ni baina ya 10-30 kwa vipimo vya knots katika maji ya Kenya na Tanzania,” alionya Dkt Gikungu.

“Mawimbi yatakuwa na urefu wa kati ya mita 1.5 hadi 3.6, yakiunda hali ya bahari ya wastani hadi nguvu.”

Kaunti zinazotarajiwa kukumbwa na hali mbaya ni pamoja na Kisumu, Homa Bay, Siaya, Migori, Busia, Kisii, Nyamira, na Nandi.

Kaunti za pwani za Mombasa, Tana-River, Kilifi, Lamu, na Kwale pia zinatarajiwa kuathirika sana.

Mjini Mombasa, Kiembeni, na sehemu za Kaunti ya Kilifi kama vile Takaungu, tayari zinahisi athari za upepo mkali uliosababisha kung’oka kwa miti.

“Upepo wa wastani hadi mkali wenye kasi ya 10 hadi 30 knots unatarajiwa, na mawimbi yanaweza kufikia urefu wa futi 12. Hali hizi zina hatari kubwa kwa vyombo vidogo na shughuli za baharini kwa ujumla,” alionya Dkt Gikungu.

Umma pia unashauriwa kuendelea kupata taarifa kupitia masasisho ya mara kwa mara kutoka kwa idara hiyo na mamlaka za mitaa.

Tahadhari hii inatolewa wiki chache tu baada ya kimbunga Hidaya.

[email protected]