Habari za Kitaifa

Wanafunzi wa Hillside Academy walikufa kwa makosa ya mtu au ajali?


ITACHUKUA muda kwa wazazi wa wanafunzi walioangamia au kujeruhiwa katika mkasa wa moto ulioteketeza bweni la shule ya Hillside Endarasha Academy, Kaunti ya Nyeri kujua kilichosababisha kisa hicho huku maswali yakiibuka kuhusu iwapo kuna mtu aliyefeli kutekeleza wajibu wake.

Wanafunzi 17 walichomeka kiasi cha kutotambuliwa na 14 wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha kufuatia mkasa huo wa moto ulioanza saa tano na dakika 35 Alhamisi usiku, Septemba 5, 2024.

Maafisa wa usalama na elimu walisema bweni la wavulana lilikuwa na wanafunzi 152 wakati moto ulipotokea katika shule iliyo na wanafunzi 824.

Huku polisi wakichunguza kilichosababisha moto huo na serikali ikiahidi kuhakikisha ukweli umejulikana, imeibuka kuwa bweni walimokuwa wakilala wanafunzi hao lilikuwa limejengwa kwa mbao na wachunguzi watalenga kubaini iwapo viwango vya ubora wa miundombinu katika taasisi za masomo ulikuwa umezingatiwa.

Ikizingatiwakuwa baadhi ya wanafunzi waliokuwa katika bweni hilo walifanikiwa kunusurika bila majeraha, wachunguzi watalenga kujua iwapo viwango vya usalama vya ujenzi wa bweni vilikuwa vimezingatiwa.

Taifa Dijitali ilibaini kuwa jengo la bweni halikuwa la kudumu.

Rais William Ruto aliagiza idara zinazohusika na usalama kuchunguza kisa hicho na kutoa usaidizi wa familia zilizoathiriwa japo ni vigumu kuziondolea uchungu wa kupoteza watoto wasiokuwa na hatia.

Haikubainika mara moja iwapo kulikuwa na walinzi na walimu katika shule hiyo ikizingatiwa ni ya msingi.

“Wizara ya Elimu inasaidiana na Wizara ya Masuala ya Ndani na Wizara ya Elimu kuhakikisha wanafunzi waliojeruhiwa wanapata matibabu bora. Wizara ya Elimu inashirikiana na mashirika ya usalama kufanya uchunguzi kubaini hasa kilichosababisha mkasa huu wa moto katika shule hii,” alisema Katibu wa Elimu ya Msingi Dkt Bellio Kipsang.

Wakazi na wazazi walisema kwamba moto huo ulianza mwendo wa tano usiku na wazima moto wa Kiawara wakajaribu kuuzima kabla ya kuzidiwa na kuomba usaidizi kutoka Huduma ya Zima Moto ya Mji wa Nyeri.

Kulingana na wakazi, zima moto kutoka serikali ya kaunti walifika mwendo wa saa tisa usiku, huku gavana wa Kaunti ya Nyeri, Mutahi Kahiga akisema hawakuweza kufika kwa wakati kutokana na matope.

Kamishna wa Kaunti ya Nyeri, Pius Murugu, alisema kuwa baadhi ya wanafunzi walioteketea watatambuliwa kupitia uchunguzi wa DNA kwa kuwa walichomeka kiasi cha kutotambuliwa.

“Wakati huo huo, usimamizi wa shule na Shirika la Msalaba Mwekundu nchini wanatafuta baadhi ya wanafunzi ambao walidaiwa kuchukuliwa na wazazi wakati wa moto huo, kwani hatujaweza kuwatambua wote,” akasema Bw Murugu.

Pia, alithibitisha kuwa Shirika la Msalaba Mwekundu linatoa ushauri nasaha kwa wanafunzi walionusurika pamoja na familia zilizoathiriwa.

Mratibu wa shirika hilo, Kanda ya Kati, Bi Esther Chege, alitaja kisa hicho kuwa cha kuhuzunisha na akahakikishia familia zote zilizoathiriwa kuwa zitapata usaidizi unaohitajika.

“Inahuzunisha sana hili limetokea, tuko hapa kutoa msaada, tutatoa ushauri nasaha hadi tutakapomaliza oparesheni hii. Tunatoa ushauri nasaha kwa wazazi, wanafunzi na jamii,” alisema.

Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki alisema kwamba wapelelezi watafanya uchunguzi wa kitaalamu kubaini kilichosababisha moto huo.