Makala

Washiriki wa Olimpiki wapewa fursa ya kutongozana bila malipo

Na GEOFFREY ANENE July 28th, 2024 1 min read

KAMPUNI ya mahaba ya Social Discovery Group (SDG) imewapa karibu wanamichezo 10,500 kutoka timu 206 fursa murwa ya kuchumbiana bila kulipia huduma za tovuti yake ya Dating.com wakati huu wa Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.

Kenya inawakilishwa na wanamichezo 70 kwenye michezo hiyo ambayo waandalizi tayari wamesambaza kondomu 200,000.

Wakenya wameingia katika fani za raga (wanaume), voliboli (wanawake), uogeleaji (wanaume na wanawake), judo (wanawake), uzio (wanawake) na riadha (wanaume na wanawake).

Dating.com inaeleza kuwa inatambua kuwa wanamichezo wanahisi wana upweke wakati wa michezo hiyo na inawasaidia kupata uhondo wa nje ya uwanja.

Tovuti hiyo inasema kuwa wanaolimpiki hao wanaweza kuwasiliana na kuendeleza mahusiano muhimu bila ya kupoteza umakinifu wao kwenye fani wanazoshiriki.

“Wanamichezo wanaweza kujiandikisha katika tovuti yetu Dating.com/Paris2024. Baada ya kuthibitisha habari zao, uanachama wao utafanywa hai na wanaweza kuanza kurusha chambo na kuunganika na wenzao wakifanikishwa na vifaa vya mawasiliano vya Dating.com, hasa Let’s Mingle,” ikasema kampuni hiyo ambayo watu 500 milioni wanatumia bidhaa zake 66.

Uamuzi wa kuanzisha mradi huo, Dating.com inasema kuwa unafuatia habari kuwa wanamichezo wako huru kuendeleza miereka ya chumbani kwenye michezo hiyo inayofanyika Julai 24 hadi Agosti 11.

Hii ni tofauti na makala yaliyopita jijini Tokyo nchini Japan wakati masharti yalikuwa makali ya kutokaribiana kwa sababu ya janga la ugonjwa wa Covid-19.

SDG inasema ni muhimu watu kutangamana na kuwa Dating.com inawapa mahali pazuri pa kufanya hivyo.

Kondomu zimekuwa zikisambazwa kwenye Olimpiki tangu mwaka 1988 jijini Seoul, Korea Kusini. Olimpiki za Seoul zilishuhudia kondomu 8,500, zikaongezeka hadi 50,000 wakati wa Olimpiki za 1992 jijini Barcelona, Uhispania.

Idadi ilikuwa 15,000 mjini Atlanta, Amerika (1996), 90,000 mjini Sydney, Australia (2000), 130,000 mjini Athens, Ugiriki (2004), 100,000 mjini Beijing, Uchina (2008), na 150,000 mjini London, Uingereza (2012).

Olimpiki za Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016 ziliweka rekodi ya dunia ya kondomu 450,000. Makala ya 2020 mjini Tokyo yalishuhudia washiriki wakipewa kondomu 160,000, lakini kama zawadi baada ya mashindano waende watumie makwao.