Habari

Wawika nje, baridi bungeni

June 23rd, 2019 2 min read

Na NYAMBEGA GISESA

WABUNGE 13 hawajatoa mchango wowote kwenye mijadala bungeni zaidi ya mwaka mmoja na nusu tangu waapishwe kuhudumu baada ya uchaguzi mkuu uliopita, shirika moja la kufuatilia utendakazi wa wabunge limefichua.

Hii ni licha ya baadhi yao kutawala vyombo vya habari kwa matamshi wanayotoa kwenye mikutano ya kisiasa nje ya bunge.

Kulingana na ripoti ya Mzalendo Trust, miongoni mwa wabunge hao ni Oscar Sudi (Kapseret), Samuel Arama (Nakuru Magharibi), Aduma Owuor (Nyakach), Justus Kizito (Shinyalu), Alfred Sambu (Webuye Mashariki), Alex Kosgey (Emgwen), James Wamacukuru (Kabete) na Charles Kamuren (Baringo Kusini).

Nao Wabunge Wawakilishi wa Kaunti ambao hawajatamka lolote bungeni tangu wachaguliwe ni pamoja na Anab Mohamed (Garissa), Lilian Tomitom (Pokot Magharibi), Irene Kasalu (Kitui), Jane Wanjiku (Embu) na Jane Chebaibai (Elgeyo Marakwet).

Mbunge mwakilishi wa Wanawake Nyamira Bi Jerusha Momanyi ni miongoni mwa waliozungumza mara nane pekee bungeni.

Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa wiki hii, wabunge hao hawajatoa mchango wowote kwenye hoja au miswada iliyowasilishwa bungeni wala kutoa taarifa au malalamishi yoyote kwa niaba ya wananchi waliowachagua.

Na katika Seneti, Seneta wa Baringo, Gideon Moi na mwenzake wa Meru, Mithika Linturi ni miongoni mwa wale ambao michango yao kwa mijadala na hoja ni finyu zaidi ikilinganishwa na wenzao. Wengine ni Issa Juma Boy (Kwale), Anwar Loitiptip (Lamu), Philip Mpaayei (Kajiado), Abdullahi Ibrahim (Wajir) na maseneta maalumu Millicent Omanga, Christine Gona, Mercy Chebeni, Victor Prengei na Falhada Dekow.

“Ajabu ni kwamba, baadhi ya wabunge na maseneta wanyamavu ukumbini ndio wanaozungumza zaidi nje ya bunge.

Miongoni mwao ni Mbw Sudi, Arama, Kizito, Linturi, Moi na Bi Omanga,” Mkurugenzi Mkuu wa Mzalendo Trust, Caroline Gaita aliambia Taifa Jumapili.

Shirika hilo limekuwa likifuatilia utendakazi wa wabunge tangu 2014, kama njia ya kuwasaidia wananchi kubaini wabunge wazembe na wale wachapa kazi ikizingatiwa kuwa wanapokea mishahara na marupurupu ya juu.

“Vilevile, matokeo ya uchunguzi yanalenga kuwapa wabunge shime ya kuzingatia wajibu wao katika utungaji sheria, uwakilishi na uchunguzi wa asasi za serikali,” akaongeza Bi Geita kuhusu ripoti hiyo ya kwanza tangu bunge la 12 lianze kazi.

Wale shupavu

Ripoti hiyo pia iliorodhesha wabunge ambao huchangia mara nyingi bungeni kuashiria kuwa ndio wachapakazi shupavu.

Wao ni Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Joseph Limo (Kipkelion Mashariki), Robert Pukose (Endebess), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Chris Wamalwa (Kiminini), James Nyikal (Seme) na TJ Kajwang’ (Ruaraka).

Kando na Nyikal na Kajwang wengine wanashikilia nafasi za uongozi katika kamati za bunge.

Wabunge wengine ambao huchangia mara nyingi kwenye mijadala bungeni ni William Cheptumo (Baringo Kaskazini), David Pkosing (Pokot Kusini), Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Paul Koingange (Kiambaa), Makali Mulu (Kitui ya Kati), William Kisang (Marakwet Magharibi) na Mbunge wa Funyula Wilberforce Ojiambo.

Na kulingana na ripoti hiyo, wabunge na maseneta vijana ambao hunawiri zaidi ni Johnson Sakaja (Seneta, Nairobi), Samson Cherargei (Seneta, Nandi), Aaron Cheruiyot (Seneta, Kericho) na Didmus Barasa (Mbunge, Kimilili).

Katika tapo la wabunge wanawake wenye umri mdogo, wachapa kazi ni; Naisula Lesuuda (Samburi Magharibi), Catherine Waruguru (Mbunge Mwakilishi, Laikipia), Martha Wangari (Gilgil) na Fatuma Gedi (Mbunge Mwakilishi, Wajir).

Wengine ni pamoja na Wabunge wawakilishi wa Kaunti; Gladys Wanga (Homa Bay), Ruweidha Obbo (Lamu), Rehema Jaldesa (Isiolo) na Faith Wairimu (Nyeri).

Maseneta walioorodheshwa kama wachapa kazi ni; Bw Sakaja (Nairobi), Moses Wetangula (Bungoma), Ledama Olekina (Narok), Samson Cheragey (Nandi), Aaron Cheruiyot (Kericho), Ephraim Maina(Nyeri), Moses Kajwang( Homa Bay), Fatuma Dullo(Isiolo), Cleophas Malala(Kakamega) na Kitui’s Enoch Wambua.

Nao maseneta maalum ambao wameonyesha utandakazi mzuri ni; Abshiro Halake (KANU), Mary Senata (Jubilee), Getrude Musuruve (ODM), Farhiya Ali (Jubilee), Agnes Zani (ODM), Isaac Mwaura (Jubilee), Naomi Waqo (Jubilee), Naomi Shiyonga (ODM), Alice Chepkorir(Jubilee) na Seneta mteule wa ANC Petronila Were.