Habari za Kaunti

Wazazi wa Isongo washtakiwa kwa kuvuruga amani shuleni

January 25th, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

WAZAZI wanne wa wanafunzi wa Shule ya Upili St Gabriel Isongo, wamefikishwa katika mahakama ya Mumias kufuatia maandamano ya Januari 12, 2024, ambayo yalilenga kumtimua mwalimu mkuu.

Mabw Amos Kweyu, Eddy Maende, Elphas Obongita, na Vincent Shiundu walisomewa mashtaka ya kumshambulia na kumsababishia majeraha mwalimu mkuu David Wafula.

Hakimu Mwandamizi wa Mumias Marcela Onyango pia aliwasomea shtaka la kuzua vurugu katika shule katika hali ambayo ilivuruga amani shuleni humo.

Wanne hao walikamatwa baada ya kizaazaa kushuhudiwa shuleni humo, wazazi wakilalamika kwamba matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023) yalikuwa ya kuaibisha.

Mahakama iliambiwa Jumanne kwamba wanne hao pamoja na wengine ambao hawakuwa kortini, waliingia shuleni kwa lazima na kumfurusha mwalimu mkuu na mkuu wa ratiba za masomo.

Inadaiwa walitenda makosa hayo Januari 12, 2024.

Walikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa bondi ya Sh50,000 au pesa taslimu Sh15,000 kila mmoja.

Kesi itatajwa Februari 2, 2024, na kusikilizwa Machi 18, 2024.

Mara baada ya tukio hilo Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) iliwaondoa walimu 17.

Baada ya wazazi wengi kuililia, iliamua kuwatuma upya walimu 17 ambapo watatu walikuwa ni kutoka kwa kundi lile lililoondolewa.

Hii ina maana kwamba TSC ilipeleka huko walimu wapya 14.

Mkurugenzi wa TSC Magharibi mwa Kenya Joseph Mugele hao watatu walikuwa wa kuwapa mwongozo walimu wapya waliofika shuleni humo ili wajifahamishe na mengi.

Naibu Kamishna wa Mumias Mashariki John Lang’at alisema walishauri wasimamizi wa shule hiyo kuweka ua wa seng’enge.

“Tumejadiliana na wanasiasa wa eneo hilo na kuwaambia waepuke vitendo vinavyohujumu shughuli za masomo,” Bw Lang’at akasema.

Alisema walimu na wanafunzi watapewa ushauri nasaha.

[email protected]