• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
Wazee Kisumu wataka serikali iwarejeshee joka lao la Omieri

Wazee Kisumu wataka serikali iwarejeshee joka lao la Omieri

Na ELIZABETH OJINA

WAZEE kutoka eneobunge la Nyakach, Kaunti ya Kisumu sasa wanataka serikali irejeshe mabaki ya joka maarufu tena la kitamaduni kwa jina Omieri ambayo yanaendelea kuhifadhiwa katika makavazi ya kitaifa jijini Nairobi.

Wakizumgumza na Taifa Leo, wazee hao wakiongozwa na mratibu wa baraza lao la maendeleo Prof Raphael Kapiyo walilalamika kwamba wameirai serikali iwarejeshee mabaki ya joka hilo bila mafanikio.

“Tumeandikia usimamizi wa makavazi ya kitaifa na Wizara ya Utalii mara nyingi ili mabaki ya Omieri yahifadhiwa hapa Nyakach kwa kuwa ni sehemu kubwa ya historia ya jamii ya Waluo,

“Hatuelewi kwa nini mabaki ya joka hilo yaendelee kuhifadhiwa Nairobi ilhali ni joka letu na lilikuwa likiishi hapa. Serikali iingilie kati na turejeshewe joka hilo tuishi nalo hapa kwa kuwa ni sehemu ya historia yetu,” akasema Prof Kapiyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno, Kaunti ya Kisumu.

Mwenyekiti wa baraza la maendeleo la wazee hao Ismail Obuom naye alisema wakazi wa Nyakach tayari wametenga ekari tatu za ardhi kujenga makao ya kisasa ya kuhifadhi joka hilo.

“Ardhi tayari ipo na tunataka serikali ijenge makao ya kisasa ya kusitiri Omieri ili iwe kivutio cha watalli,” akasema Bw Obuom.

Mara ya mwisho ambapo wakazi wa Kisumu waliyaona mabaki ya joka hilo ni mnamo 2018 yalipoletwa katika uwanja wa Jomo Kenyatta ambao kwa sasa unajulikana kama uga wa Jaramogi Oginga Odinga jijini Kisumu.

Omieri alikufa mnamo Julai 9, 1987 baada ya kuteketea vibaya kwenye kisa cha moto ndani ya msitu moja eneo la Nyakach.

You can share this post!

Ni kubaya 2022!

‘Tuliangusha BBI kuadhibu gavana’