Habari za Kitaifa

Wazee wamtaka Omar kufyata ulimi, akome ‘kuchimba’ Gachagua baada ya kukalia kiti UDA

Na MWANGI MUIRURI September 5th, 2024 2 min read

WAZEE kutoka eneo la Mlima Kenya wanamtaka Rais William Ruto kumshauri Katibu Mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Hassan Omar akome kumshambulia kila mara Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Ndani ya kipindi cha majuma mawili yaliyopita, Bw Omar ametoa taarifa mara mbili akimshutumu Bw Gachagua, hali inayowakera aliyekuwa mkuu wa mkoa Joseph Kaguthi na mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu Wachira Kago.

Wengine waliokasirishwa na shutuma ambazo Omar anamwelekezea Gachagua ni Mwenyekiti wa Gema Lawi Imathiu na mdhamini wa kitaifa wa baraza la “Kiama Kia Ma” Kung’u Muigai.

Bw Omar amewashutumu wandani wa Naibu Rais waliolalamikia hatua ya Rais William Ruto kukutana na baadhi ya wabunge kutoka Mlima Kenya bila kuwepo kwa Bw Gachagua.

Mwakilishi huyo wa Kenya katika bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alisema Naibu Rais siye “mwenye ufunguo wa Mlima Kenya” .

“Rais anaweza kukutana na kiongozi yeyote anavyotaka. Mtu fulani hafai kuendeleza dhana kwamba sharti rais apate kibali kutoka kwake kabla ya kukutana na viongozi wa Mlima Kenya. Kenya ina Rais mmoja sio marais wawili,” Bw Omar akasema.

Mnamo Jumapili wiki jana (Agosti 24, 2024), Bw Omar alijitokeza tena, akimtaja kama “anayejifanya kuwa mfalme wa Mlima Kenya na kiongozi anayeendeleza siasa kutenganisha na asiyekumbatia wengine.”

Hata hivyo, wazee wa Mlima Kenya wamemkaripia vikali Katibu huyo Mkuu wa UDA kwa kumkosea heshima Bw Gachagua ambaye ni naibu kiongozi wa kitaifa wa chama hicho.

Wanasema Bw Omar pia alikuwa mstari wa mbele kupinga pendekezo la Bw Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wa Hayati Mwai Kibaki 2013.

“Huwa sipendi kujiingiza katika makabiliano, lakini huyu mtu anayeitwa Omar amevuruga uvumilivu wangu. Kiongozi wa hadhi ya Naibu Rais anafaa kuheshimiwa na yeyote yule, haswa viongozi kama Omar wanaoshikilia nyadhifa za juu katika chama tawala cha UDA,” akasema Bw Kaguthi.

“Katika siku za hivi karibuni Bw Omar amekuwa akirusha maneno yasiyo ya heshima upande wa Bw Gachagua, hali inayotufanya kujiuliza anakopata ujasiri wa kufanya hivyo,” akaeleza.

Tulipofikia Bw Omar kuhusu suala hili alijibu hivi: “Nitahitaji kutafakari tena. Huenda nilikosea katika ufasiri wangu.”

Alisema anashangaa kuwa kauli zake “za nia njema” hufasiriwa kama za chuki.

“Sitaki kusema zaidi ya hapo,” akaongeza Bw Omar, ambaye ni Seneta wa zamani Mombasa.

Bw Kiago aliambia Taifa Dijitali kwamba “Kupitia kauli zake za kuanzia mwaka wa 2013, Bw Omar amekuwa akiendeleza umoja wa watu wa Mlima Kenya. Japo kauli zake za juzi zinamkosea heshima Bw Gachagua, na naibu rais anachangia kuleta umoja wetu kama watu wa eneo anakotoka.”

Alisema kuwa 2013 wazee wa Mlima Kenya walikutana mjini Limuru (Kongamano la Limuru II) na wakamwidhinisha Bw Kenyatta kuwania urais.

“Lakini Bw Omar alitumiwa na watu akidai kuwa baada ya Mwai Kibaki kukamilisha mihula yake miwili, kiti cha urais kilifaa kuendea mtu kutoka jamii zingine,” Bw Kiago.