HabariHabari za Kitaifa

Waziri mteule akiri kutokuwa na ufahamu wa majukumu ila atajifunza

Na NDUBI MOTURI August 10th, 2024 1 min read

WAZIRI Mteule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Maendeleo ya Maeneo Kame, Beatrice Askul, amekiri kuwa haelewi masuala ya Wizara aliyoteuliwa kuongoza.

Akijitetea mbele ya Bunge la Kitaifa Ijumaa Agosti 9, 2024 Bi Askul , alisema kuwa ana uwezo wa kujifunza kila kitu kinachohusiana na Wizara hiyo atakapoidhinishwa.

“Nilikuwa na siku nne tu za kusoma na kujifunza zaidi kuhusu EAC kwani sina ufahamu zaidi kuhusu masuala ya wizara niliyoteuliwa kuiongoza. Mara tu nitakapoidhinishwa, nitajifunza kwa kuwa mimi ningali mchanga na nitatumia uzoefu wangu kuongoza wizara, ” alisema.

Bi Askul ambaye anatazamiwa kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Turkana kushikilia wadhifa huo ikiwa ataidhinishwa na Bunge la Kitaifa, alisema atazingatia matumizi ya teknolojia na utekelezaji wa miradi ya miundombinu kutatua matatizo ya muda mrefu ya Kenya kama vile foleni ndefu mipakani.

“Tunahitaji kuharakisha maendeleo ya miundombinu na teknolojia. Tunahitaji kushirikiana kama serikali na kutafuta suluhu. Tunahitaji kutenga fedha na kutekeleza miradi ambayo itawezesha usafirishaji wa bidhaa na huduma,” aliambia Kamati ya Uteuzi iliyoongozwa na Spika Moses Wetang’ula.

Kuhusu suala tata la Kisiwa cha Migingo, Bi Askul alisema ni lazima Uganda na Kenya ziwe na mazungumzo.

“Napendekeza tutatue suala hilo kupitia Mahakama ya Haki ya Tanzania. Tunahitaji pia kuwa na waamuzi wasioegemea upande wowote ili kutatua suala hilo. Ikiwa hatutapata suluhu, Wakenya wengi zaidi watateseka,” aliongeza.

Bi Askul aliwahi kuhudumu katika wadhifa wa Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maji eneo la Bonde la Ufa.

Waziri huyu mteule alipendekeza matumizi ya mikakati endelevu na madhubuti kukabili majanga kama vile ukame na mafuriko.

“Wacha tutumie ripoti za hapo awali kufanya uamuzi. Tunahitaji kufanya kazi na washirika kuja na miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” akaongeza.