Habari za Kitaifa

Weta naye asalimu amri ya Gen Z kwa kuzima mikutano katika mikahawa ya kibinafsi


KWA hofu ya “kusalimiwa” tena na vijana wa Gen-Z baada ya “salamu” za Juni 25, 2024 Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amepiga marufuku mikutano ya kamati kufanyika katika mikahawa ya kibinafsi.

Kwenye taarifa aliyotoa Ijumaa, Julai 13, 2024 Bw Wetang’ula aliziamuru kamati zote za bunge kufanya mikutano yao katika vyumba vya kamati katika majengo ya bunge ili kupunguza matumizi ya pesa za umma.

“Ikiwa vyumba katika majengo ya bunge havitatosha kamati za bunge zinaagizwa kuendesha vikao vyao katika majumba ya serikali wala sio katika mikahawa ya kifahari ya kibinafsi,” Bw Wetang’ula akaeleza.

Agizo lake linajiri wiki moja baada ya Rais William Ruto kutangaza mikakati kadhaa ya kupunguza matumizi ya fedha serikali kuafiki mojawapo ya matakwa ya Gen Zs kwamba serikali ipunguze ubadhirifu.

Ubadhirifu wa pesa za umma, ufisadi, ushuru wa juu, utawala mbaya na ukosefu wa ajira ni miongoni mwa matakwa ambayo vijana hao na yalipelekea wao kuandamana kuishinikiza serikali itekeleze.

Hii ni kando na Mswada wa Fedha wa 2024 ambao hatimaye Rais Ruto aliuondoa na kuamuru kwamba wabunge waufutuliwe mbali kabisa.

Miongoni mwa mikahawa ya kibinafsi ambayo kamati za bunge la kitaifa na seneti zilipenda kuendeshea vikao vyao ni pamoja na; Boma iliyoko mtaa wa  South C, Weston inayohusishwa na Rais Ruto, Hilton Garden Inn, na Windsor Golf Hotel iliyoko Kiambu.

Mingine ni; mkahawa wa Ole Sereni ulioko Mombasa Road, Eka Hotel, Panari, Tamarind, Trademark, Radisson Blu, Four Points Sheraton, Sarova Panafric, yote iliyoka viungani wa jiji la Nairobi.

Kamati hizo zilikuwa zikiendelea kuanda mikutano katika mikahawa hiyo hata baada ya Rais Ruto kuzindua rasmi jengo jipya la Bunge Towers mnamo Mei 23, 2024. Jengo hilo ambalo ujenzi wake uligharimu Sh9.5 bilioni, pesa za umma linasheheni vyumba vingi vya mikutano na afisi za wabunge na maseneta.

Akiongoza hafla ya ufunguzi rasmi wa jengo hilo, Rais Ruto alisema matumizi yake yataiwezesha serikali kuokoa takriban Sh440 milioni ambazo zilikuwa zikitumika kila mwaka kukodisha afisi za wabunge na vyumba vya kufanyia mikutano.