Habari za Kitaifa

Wildlife Works yatoa Sh70m kuwapiga jeki wanafunzi 6,695 Taita Taveta

June 7th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

WANAFUNZI 6,695 kutoka Kaunti ya Taita Taveta wamepigwa jeki kwa kukabidhiwa basari ya kima cha Sh70 milioni kutoka kwa shirika la Wildlife Works Community linaloshughulika na masilahi ya wanyamapori, utunzaji misitu na harakati za kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Basari hizo zimewafaidi wanafunzi wa shule za sekondari na pia taasisi za kitaaluma na vyuo vikuu na ambapo kutoka mwaka wa 2012, kitita ambacho shirika hilo limetoa kwa wenyeji hao ni Sh273 milioni kwa manufaa ya wanafunzi 43,837.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mawasiliano wa shirika hilo Bw Joseph Mwakima, walionufaika walitambuliwa kupitia bidii na uadilifu wa kamati maalum zilizo katika mashinani na ambapo katika kiwango cha wadi, walengwa wote walitambuliwa huku walio na ulemavu na wale ambao ni mayatima wakipewa kipaumbele.

“Waliotambuliwa walitoka kutoka lokesheni za Mwatate, Mwachabo, Marungu, Kasigau, Mackinnon na Sagalla na walipokezwa hundi zao katika hafla ya Juni 6, 2024, ambayo mgeni wa heshima alikuwa ni Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime,” akasema Bw Mwakima.

Kupitia taarifa kwa waandishi wa habari, Bw Mwadime alishukuru shirika hilo akisema jeki hiyo ya basari itawafaa walionufaika kwa kiwango kikuu.

“Mchango huu ni wa maana sana kwa kuwa unalenga kuwapa wanafunzi wetu wa kutoka familia maskini lakini werevu na wenye bidii, makali ya elimu na ambayo ndio urithi wa maana zaidi ambao tunaweza kama jamii na washirika wetu tukawatuza,” akasema.

Aliongeza kwamba elimu huchangia pakubwa kuimarika kwa maisha ya watoto na kuwapa makali ya kupambana na hali za baadaye katika maisha ikizingatiwa kwamba kaunti hiyo haina ule upana wa kuwahami wote.

“Elimu inatupa nafasi za kutoka nje ya mipaka yetu kwenda kupambania nafasi za kiriziki kwingineko,” akasema.

Bw Mwakima aliwapongeza wenyeji kwa kuwa marafiki wa mazingira na pia ushirika wao mwema katika kufanikisha uhusiano wao na mashirika yote ambayo huzingatia usafi na usalama wa mazingira.