Habari za Kitaifa

Zabuni ya cherehani yatishia kummeza mkuu wa taasisi ya mafunzo ya kiufundi

June 4th, 2024 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Utoaji Mafunzo ya Kiufundi ya Kitaifa (NITA) Stephen Ogenga Jumatatu alishtakiwa kwa ufujaji wa Sh4.8 milioni katika zabuni ya cherehani.

Ogenga alishtakiwa pamoja na wakurugenzi wawili wa kampuni Xponics James waweru and Sheila Wambui Nyakinyua mbele ya hakimu mkazi Ziporah Gichana.

Waweru na Nyakinyua walishtakiwa kwa uporaji wa Sh10,189,064.

Wawili hao walidaiwa waliwasilisha zabuni feki Nambari NTA/12/2017-2018 ya kuuzia NITA cherehani.

Shtaka liliendelea kusema wakurugenzi hao walidai walikuwa wamepewa kandarasi ya kuuza, kutengeneza na kurekebisha cherehani zilizoharibika katika shirika hilo la NITA.

Mahakama ilielezwa kwamba washtakiwa hao walikula njama za kufuja shirika hilo kati ya Aprili 15 2019 na Juni 30, 2021.

Bi Gichana alielezwa kuwa Waweru na Nyakinyua walidanganya walikuwa wameteuliwa na NITA kuliuzia cherehani na kutengeneza zile zilizoharibika.

Waweru na Nyakinyua walishtakiwa kutumia zabuni feki kupokea pesa za umma Sh10,189,064.

Ogenga alikana kutumia mamlaka yake vibaya kwa kuidhinisha Xponics ilipwe Sh4,800,654 kwa madai iliteuliwa kuuzia NITA cherehani.

Mshukiwwa mwingine Paul Kipsang Kosgei hakufika kortini kujibu shtaka la kutumia mamlaka yake vibaya alipokuwa Mkurugenzi Mkuu wa NITA.

Shtaka lilisema Kosgei aliidhinisha Xponics Ltd ilipwe Sh5,388,410 kwa kuuzia NITA cherehani kati ya Januari 31 na Machi 29, 2019.

Hakimu alielezwa Kosgei hakujua alitakiwa kufika kortini Jumatatu kujibu shtaka.

Korti ilielezwa anaishi mashambani na akipewa muda atasafiri hadi Nairobi kujibu shtaka dhidi yake.

Hakimu aliamuru mshtakiwa huyo afike kortini Juni 5, 2024 kusomewa shtaka na kulijibu.

Ogenga, Waweru, Nyakinyua na Xponics waliomba waachiliwe kwa dhamana.

Upande wa mashtaka haukupinga ombi hilo.

Washtakiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni ama walipe pesa tasilimu Sh1 milioni ndipo waachiliwe kutoka kizuizini wafanye kesi wakiwa nje.

[email protected]