Mashairi

SARATANI WATUTAKIANI?

July 29th, 2019 1 min read

NA NEHEMIAH OMUKONYA

Ninaandika, chozi likinidondoka,
Nahuzunika, wapendwa tukiwazika,
Hapa nataka, ‘jua tutavyoepuka,
Saratani! Tukupe nini utuache?

Hapa twateta, jinsi umetutenda,
Ushamchota, jatelo tulompenda,
Na umekita, kambi hutaki kuenda,
Saratani! ‘Takupani ujiondoe?

Madaktari, mkazo wakutilia,
Kwenye kaburi, wengi umeshindilia,
Na kwa kiburi, katufanya wa kulia,
Saratani! Ni kipi unachotudai?

Watuandama, kama kwako tulikopa,
Tutasimama, hadi utakaposepa,
Hatutakoma, kiapo hiki twaapa,
Saratani! Hadi lini ukitufwata?

Na kumaliza, ni kwa hili ombi moja,
Namuuliza, Mola aone twangoja,
Kwa muujiza, afanye tupate hoja,
Saratani! ‘Tatuambia watakani?

Malenga Mukonya Mukonya