Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Je, washangaa kwa nini mende wameganda kwako?

July 30th, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

UNAPOPITA mitaani hasa jijini Nairobi, hutakosa kusikia wachuuzi wakiita wateja kununua dawa ya mende; “Dawa ya mende, angamiza mende”.

Umewahi kununua dawa hizo lakini ungali unasumbuliwa na mende?

Utafiti wa kimatibabu uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa dawa zinazouzwa mitaani au madukani zimepoteza makali ya kuua mende.

Wanasayansi wanasema kwamba tayari miili ya wadudu hao imezoeana na dawa zilizoko sokoni hivyo haziwezi kuwadhuru. Watafiti wanasema dawa zinazotumiwa sasa zinasambaza tu mende kwa majirani badala ya kuwaua.

Wanasema sasa wana ushahidi kwamba itakuwa vigumu kuua mende kwa kutumia dawa zilizopo madukani.

Utafiti huo uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Purdue, Amerika, ulihusisha mende aina ya Blattella germanica ambao pia hupatikana kwa wingi humu nchini, kulingana na Kituo cha Kimataifa kuhusu Utafiti wa Wadudu (icipe), Kenya.

Blattella germanica ni aina ya mende ambao wamekuwa wakihangaisha mamilioni ya watu kote duniani.

Aina nyingine za mende ambao huhangaisha watu nchini Kenya ni Blatta orientalis, Periplaneta Americana na Supella longipalpa, kulingana na icipe.

Mtafiti mkuu Michael Scharf alisema kuwa mende walianza kuzoeana na dawa tangu miaka ya 1950. Hiyo inamaanisha kwamba dawa zinazotengenezwa huua mende kwa muda mfupi na kisha kukosa makali. “Kila mara dawa mpya inapotolewa, hufanya kazi kwa muda mfupi na kisha kuzoeana na mende,” wakasema watafiti hao.

Nchini Kenya, Dkt Chrysantus Mbi Tanga, mtafiti wa wadudu katika kituo cha ICIPE anasema kuwa tatizo la mende kuzoeana na dawa ni changamoto kubwa humu nchini. “Hiyo ndiyo changamoto kubwa inayotukumba sisi wanasayansi nchini Kenya. Wakenya wamekuwa wakitaka tuwaeleze dawa ifaayo kwa sababu zile wanazotumia hazifanyi kazi,” akasema.

Mende ni hatari kwa afya. Mende hubeba bakteria hatari kama vile ‘Salmonella’, ‘Enterococcus’ ambao husababisha maumivu ya tumbo na kuhara, kipindupindu na hata kichocho.

Kubeba mamia ya bakteria

Kwa mujibu wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Purdue, mende aina ya Blattella germanica wana uwezo wa kubeba mamia ya bakteria.

Mende hao huzunguka kote ndani ya nyumba kutoka chooni hadi jikoni na hata katika debe la kuhifadhia unga. Wadudu hao huacha bakteria hao hatari kila mahali wanapopitia.

Ripoti ya watafiti hao inasema kuwa kinyesi cha mende hao pia husababisha maradhi ya pumu (asthma).

“Kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha uhusiano baina ya bakteria wanaoenezwa na mende na maradhi ya pumu. Mende husababisha kuwepo kwa chembechembe za vumbi ndani ya nyumba hivyo kusababisha maradhi haya,” inasema ripoti hiyo.

Kulingana na Bodi ya Kukabiliana na Wadudu nchini, kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za mende ni Pyrethroid, Pyrethrin, Boric acid, Fipronil, Carbamates Diazinon, Carbaryl, Chorpyrifos-methyl na Pirimiphos-methyl.

Watafiti nchini Amerika walitumia kemikali hizo katika utafiti huo ambapo walibaini kwamba hazikuweza kuua hata mende wadogo wanaozaliwa.

Mende mmoja jike aina ya Blattella germanica anazaa hadi watoto 40 kila baada ya miezi michache.

Watafiti wanasema kuwa kuangamiza mende hao itakuwa vigumu kutokana na ukosefu wa dawa thabiti. Sasa wanasayansi hao wanataka watu kudumisha usafi ndani ya nyumba na mazingira yanayowazunguka kama njia mojawapo ya kupunguza mende. “Ni heri kudumisha usafi wa mazingira ndani na nje ya nyumba kuliko kupoteza hela nyingi kununua dawa ambazo hazitakusaidia,” anasema Scharf.

Wanasayansi pia wanaonya kuwa kutumia kemikali nyingi kupita kiasi katika harakati za kukabiliana na mende ni hatari kwa mazingira. Dkt Tanga anasema wanasayansi katika kituo cha icipe wanaendelea kufanya utafiti kwa lengo la kupata dawa itakayoangamiza mende bila kudhuru mazingira.