Habari Mseto

Ruto akaidi agizo la maaskofu Wakatoliki

October 7th, 2019 1 min read

Na CHARLES WANYORO na CECIL ODONGO

NAIBU Rais William Ruto, Jumapili alionekana kukaidi agizo la maaskofu wa Kanisa Katoliki kuhusu utoaji michango kanisani.

Mnamo Jumamosi, Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB) ulitoa agizo kwamba zawadi yoyote inayozidi Sh50,000 lazima iambatanishwe na barua yenye maelezo kuhusu namna zilivyopatikana kati ya masharti mengine makali ya kutimizwa kama njia mojawapo ya kupigana na ufisadi.

Hata hivyo, Jumapili, Dkt Ruto alitoa mchango wa Sh1 milioni pesa taslimu kwa Kanisa Katoliki la Mujwa, Kaunti ya Meru.

Wasaidizi wake walikaidi wito wa parokia hiyo Enrique Rituero, kutia saini stakabadhi yenye maelezo kuhusu mchango huo kama ilivyoagizwa na KCCB.

Dkt Ruto pia alitoa michango katika Kanisa la Great Gospel Visioners International (Sh500,000) na Kamugaka Methodist (Sh1 milioni).

Katika hotuba yake, Dkt Ruto alisema wanaomwambia akome kuchangisha fedha hizo ni watu wachoyo wenye mikono gamu kwani yeye hutoa kwa hiari wala si kwa sababu za kupata umaarufu wa kisiasa.

Pingamizi

“Msiwasikize wale ambao wanapiga kelele. Ni baraka tele kutoa kwa ajili ya kazi ya Mwenyezi Mungu,” akasema Dkt Ruto.

Wakati huo huo, Tume ya Maadili na Kukabili na Ufisadi (EACC) imesifu msimamo wa Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki kuhusu utoaji michango kanisani na kupendekeza kwamba makanisa mengine yanafaa kufuata mkondo huo.

Kupitia taarifa iliyotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji Twalib Mbarak, EACC iliwasifu maaskofu hao kwa kuhakikisha kwamba kuna uwazi kuhusu maswala yote ya fedha zinazochangishwa au kutolewa kusaidia makanisa yao.

“Ni jambo la wazi kwa umma kwamba visa vya ufisadi vimefikia viwango vya kutisha nchini na wafisadi sasa wanapeleka pesa chafu kwa mashirika ya kidini hasa makanisani,” akasema Bw Mbarak.