Makala

GWIJI WA WIKI: Amondi Ochieng

August 12th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

AMINI kwamba hakuna lisilowezekana.

Jitume na ujitahidi kusonga mbele bila kukata tamaa.

Fuata msukumo wa ndani ya nafsi yako, jiwekee malengo ya mara kwa mara na ujiboreshe katika chochote unachojishughulisha nacho.

Yafanye mambo kwa utaratibu ufaao, shindana na wakati na ukithamini sana unachokifanya kwa sababu mafanikio hutegemea ukubwa wa shauku yako, kiwango cha imani yako na upekee wa ubunifu wako.

Huu ndio ushauri wa Bi Belinda Amondi Ochieng – mwandishi chipukizi na mtaalamu wa masuala ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (Teknohama) ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Premier Rajchandra Academy, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Amondi alizaliwa kijijini Kosele, Oyugis, katika eneo la Karachuonyo, Kaunti ya Homa Bay. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto wanne wa Bi Debra Achieng na Bw Joshua Ochieng.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi ya Ober, Mikayi, Homabay mnamo 1997. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya Gideons Memorial Academy, Oyugis mnamo 1999. Huko ndiko alikofanyia mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mnamo 2004.

Alijizolea alama nzuri zilizompa nafasi katika Shule ya Upili ya Asumbi Girls, Homabay mnamo 2005. Alifanya Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 2008.

Ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa na Bw Oscar Jonyo aliyemfundisha katika shule ya msingi. Mwalimu Jonyo alimpa Amondi motisha ya kupiga mbizi katika bahari ya uandishi baada ya kutambua kipaji cha utunzi ndani ya mwanafunzi wake huyu.

Ilhamu zaidi ya Amondi katika makuzi ya Kiswahili ilichangiwa na Mwalimu Herbert Busese ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Asumbi Girls. Japo matamanio ya Amondi yalikuwa ni kuzamia masomo ya Hisabati na Fikizia katika chuo kikuu, kutangamana kwake na Bw Busese kulimbadilisha mawazo na akahiari kuogelea katika bahari pana ya Kiswahili.

Hata hivyo, anasema mapenzi yake kwa sayansi yangalipo na anapania kutumia ubunifu wake katika masomo hayo kuandika kazi za kuvutia zaidi kwa Kiswahili. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kujenga upya taswira ya Kiswahili miongoni mwa vijana wanaochipukia katika taaluma mbalimbali za sanaa na sayansi.

Anaamini kwamba kila mwanataaluma anastahili kujihisi kuwa ana nafasi maridhawa ya kuchangia maendeleo ya Kiswahili badala ya jukumu hilo kuachiwa ‘Waswahili’ pekee.

Amondi alisomea Shahada ya Elimu katika Mahitaji Maalumu pamoja na masuala ya Habari na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Maseno kati ya 2010 na 2014. Ualimu wake uliegemea zaidi Kiswahili na somo la Dini.

Akiwa chuoni, alijunga na Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maseno (CHAKIMA) na akawa pia mwanachama wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA).

Zaidi ya kuchangia mashairi, makala na habari mbalimbali katika chapisho maalumu la CHAKIMA, alishiriki katika uendeshaji wa chama kikamilifu na akapata msukumo wa kuhariri miswada ya vitabu iliyotungwa na wanachama wenzake.

Alishirikiana na wanafunzi wenzake kuandaa michezo mbalimbali ya kuigiza na wakaandika ‘Miongozo’ ya vitabu teule vya fasihi vilivyokuwa vikitahiniwa katika KCSE Kiswahili miaka hiyo. Walifanya haya chini ya uelekezi wa Bw Patrick Temba wa Chuo Kikuu cha Maseno.

Amondi alikuwa pia kwenye mstari wa mbele kuwaongoza WanaCHAKIMA kuzuru shule mbalimbali za Kaunti ya Kisumu kwa nia ya kushauri, kuelekeza na kuwahamasisha wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

UALIMU

Amondi alijitosa rasmi katika ulingo wa ualimu mnamo 2014 alipoajiriwa na Shule ya Upili ya Jane Adeny katika eneo la Muhoroni, Kaunti ya Kisumu. Nafasi hiyo ilimpa mazingira faafu yaliyomwezesha kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhamia Nairobi Leadership Academy alikofundisha hadi 2018. Amewahi pia kufundisha katika Shule ya Flying Kites Leadership Academy kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Premier Rajchandra Academy, Nairobi.

Amondi amechangia makuzi ya Kiswahili shuleni Premier Rajchandra kwa njia tofauti. Alianzisha maadhimisho ya ‘Wiki ya Kiswahili’ ili kuwapa wanafunzi kutoka mataifa ya kigeni jukwaa mwafaka zaidi la kukichangamkia Kiswahili wanachokisoma kama lugha ya pili au hata ya tatu.

Masomo ya kawaida yatakaporejelewa baada ya janga la korona kudhibitiwa vilivyo humu nchini, Amondi anaazimia kuanzisha Chama cha Kiswahili kitakachowaamshia wanafunzi wake wa Premier Rajchandra Academy ari ya kuitumikisha lugha hii kwa kani na idili.

UANDISHI

Ingawa sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani ya Amondi akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi, safari yake katika ulingo huu ilianza rasmi alipojiunga na Chuo Kikuu cha Maseno mnamo 2010.

Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na upili, aliandika insha nyingi zilizomvunia tuzo za kutamanisha. Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi ya kizalendo yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali.

Mwandishi Amondi Ochieng. Picha/ Chris Adungo

Anapania kuzikusanya tungo hizo na kuchapisha diwani ambayo anaamini itabadilisha sura ya kufundishwa na kusomwa kwa Ushairi wa Kiswahili miongoni mwa walimu na wanafunzi wa shule za msingi, upili na vyuo.

Amondi kwa sasa anaandaa miswada miwili ya tamthilia na anatazamia kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi wake katika ulingo wa uandishi wa kazi bunilizi.

Kitabu chake cha kwanza kuchapishwa ni tamthilia ya ‘Kito Chenye Doa’ kilichofyatuliwa mnamo Aprili 2020. Kitabu hiki kinaangazia masuala ya uongozi pamoja na usalama wa watoto na vijana.

USALAMA WA VIJANA

Mnamo 2018, Amondi alianzisha mpango wa kuhamasisha wanafunzi wa shule za upili humu nchini kuhusu athari za mimba za mapema, masuala ya afya ya kiakili, uongozi na udhibiti wa hisia za mwili.

Anatekeleza haya kupitia mradi wa Safety for Success Education ambao umempa fursa ya kufanya kazi kwa pamoja na mashirika mbalimbali kama vile World Vision, Research Triangle Institute na East African Child Rights Trust.

MAAZIMIO

Amondi ana azma ya kufikia upeo wa taaluma yake na kuwa profesa, mhadhiri wa chuo kikuu, mmiliki wa maktaba ya Kiswahili na mwandishi maarufu wa Kiswahili pamoja na masuala ya jinsia na uana.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inawatawala walimu ambao wametangamana naye katika warsha na makongamano mbalimbali.

Amondi anawastahi sana wanafunzi wake ambao bado wanajishughulisha na Kiswahili licha ya kupata ajira katika sekta na taaluma tofauti.