Jamvi La Siasa

Raila agonga serikali licha ya kuungwa AUC

June 9th, 2024 3 min read

NA BENSON MATHEKA

JUHUDI za viongozi wa Kenya Kwanza kuzima kiongozi wa ODM Raila Odinga asikosoe serikali kwa kuwa inaunga azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) zinaonekana kugonga mwamba huku akiweka wazi kuwa hakuomba serikali imuunge mkono.

Viongozi wa serikali akiwemo kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto wamekuwa wakimtaka Bw Odinga afunge mdomo kwa kuwa serikali inamsaidia kutafuta wadhifa mkubwa wa bara.

“Kwa sasa, unachotafuta ni kazi ya AU. Watu wa Kenya hawapigii kura wadhifa huo wa AU. Masuala ya kujiingiza katika siasa ndogo kama nilivyoona ukifanya jana (Ijumaa) ndio yatakufanya ukose kazi ya AU sawa na ulivyokosa urais. Kuwa muungwana na unyamaze kabisa,” alisema Bw Cheruiyot.

Kampeni

Mnamo Jumanne wiki hii, alipokutana na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kujadili kampeni yake, Raila alisema kwamba japo anahitajika kuidhinishwa na serikali ili agombee uenyekiti wa AUC, hakutarajia imuunge mkono.

“Ulikuwa uamuzi wangu kugombea na inahitajika kupata idhini ya serikali. Nilitarajia ikatae. Nilishtuka ilikubali kuniunga mkono,” alisema.

Siku moja baada ya mkutano huo, Bw Odinga alikutana na waandalizi wa kongamano la Limuru 3 waliomkabidhi maazimio ya mkutano wao yaliyojumuisha wito wa mgao wa mapato ya serikali kwa kutegemea idadi ya watu.

Wito huo umezua mgawanyiko katika chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) Naibu Rais Rigathi Gachagua akishinikiza utumie licha ya Rais Ruto kuukataa.

Bw Odinga alimuunga Bw Gachagua akisema kuwa ugavi wa rasilmali unapaswa kutegemea idadi ya watu na sio ukubwa wa eneo.

“Ninaunga mkono ugavi wa rasilimali kwa msingi wa mtu mmoja-kura moja-shilingi moja. Ninajua baadhi ya watu hawafurahishwi na hili ila ninachoweza kusema ni kwamba huu ni mjadala muhimu tunaopaswa kushiriki kikamilifu,” akasema Bw Odinga na kusisitiza suala hilo lilikuwa mojawapo wa mapendekezo ya Mpango wa Maridhiano (BBI) alioshinikiza pamoja na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Kulingana na mbunge wa Belgut, Nelson Koech, mwandani mwingine wa Rais Ruto, Raila anafaa kufunga mdomo kwa kuwa serikali inamfanyia kampeni AUC.

“Kwa sasa tunapoongea, kampeni inaendelea ufanikiwe kuwa mwenyekiti wa AUC ambayo imepangwa na kutekelezwa na serikali. Sio haki uweze kushirikiana na watu serikalini wanaohujumu urais wa Ruto,” alisema Koech akikosoa Bw Odinga kwa kuunga Bw Gachagua.

Hata hivyo, Bw Odinga hakunyamaza na mnamo Ijumaa, alikosoa Mswada wa Fedha wa 2024 akisema utafanya Wakenya kuumia zaidi.

Soma Pia: Hatimaye Raila akohoa kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024

Kulingana na Bw Odinga, mapendekezo mengi kuhusu utozaji ushuru yaliyo katika mswada huo ni mabaya kwani hayazingatii masilahi ya wananchi wa kawaida.

“Mswada wa Fedha wa 2024 unapendekeza mfumo wa utozaji ushuru ambao hautabiriki, ni ngumu kuuelewa, hauna uwazi na hauzingatii usawa na haki. Kwa hivyo ni vigumu kutekelezwa,” akaeleza Raila.

“Mswada huu ni mbaya kuliko ule wa 2023, utaua uwekezaji na unaongeza machungu kwa Wakenya ambao walitarajia kuwa machozi yaliyowatoka kuhusiana na ushuru wa mwaka 2023 yangeisukuma serikali kuwapunguzia mzigo wa ushuru mwaka huu wa 2024,” akasema na kuwahimiza wabunge kuukataa.

Fungwa mdomo

Kulingana na wadadisi wa siasa, kauli za hivi punde za Bw Odinga zinaonekana kuondoa taswira kwamba amefungwa mdomo na serikali kwa kuwa inaunga azma yake AUC.

“Kuanzia siku aliyokosoa serikali akiwa Mukuru kusaidia waathiriwa wa mafuriko hadi aliposema kuwa yeye sio mradi wa serikali katika kuwania wadhifa AUC na kukosoa mswada wa Fedha 2024, Bw Odinga anataka kuondoa dhana kwamba ameingizwa kwenye makwapa na serikali ya Dkt Ruto ambayo alikuwa mkosoaji wake mkubwa,” asema mchambuzi wa siasa Paul Wanyama.

Anasema Bw Odinga anatuma ujumbe kwamba hajaacha kutetea raia wa kawaida na kwamba hajaacha jukumu lake kama kiongozi wa upinzani.

“Hii ndio sababu alikutana na waandalizi wa Limuru III na kupokea maazimio yao ikiwa ni pamoja na takwa la kugawa mapato ya serikali kwa kutegemea idadi ya watu,” akasema Bw Wanyama.