Akili Mali

Wajane waungana kukabiliana na njaa kupitia kilimo 

Na SAMMY WAWERU  June 25th, 2024 2 min read

MWAKA 2020, Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa ugonjwa hatari wa Covid – 19 na ni katika kipindi hicho kundi la wajane kutoka Kitui liliungana kupunguza mahangaiko. 

Hata ingawa maradhi hayo yaliyosababishwa na virusi vya Corona, ulimwengu 2022 ulitangaza kuwa huru, wengi walitatizika na isemavyo umoja ni nguvu utengano ni udhaifu; kundi hilo linalojumuisha kina mama na wazee lilithibitisha kauli hiyo.

Chini ya Wekwatio Self-Help Group, waliungana kwa lengo la kuzalisha chakula.

Elizabeth Kyalo, mwenyekiti, anasema kufuatia amri ya kuingia ama kutoka kaunti zilizotajwa kuwa hatari katika usambazaji wa Corona ambapo utoaji huduma muhimu uliathirika, wajane hasa wasio na uwezo kimapato maeneo kame walijipata kwenye njiapanda.

Kitui ni kati ya kaunti zinazoorodheshwa kama kame (ASAL) nchini.

“Masoko hayakuwa na bidhaa zote za kula na wengi wetu tulitatazika,” Elizabeth anasema.

Ikizingatiwa kuwa wengi wao hawana ajira, walikuwa na muda mwingi na mrefu wa kusalia nyumbani na mama huyu ambaye ni mjane anasema waliugeuza kuwa jukwaa la kujiendeleza.

Kundi la Wekwatio likazaliwa.

Baadhi ya wanachama wa Wekwatio Self-Help Group wakivuna mboga kwenye bustani ya mafunzo ya kundi hilo Kijiji cha Kalandini, Kitui ya Kati. PICHA|SAMMY WAWERU

Lina jumla ya wanachama 45, na kila mmoja anafanya kilimo kwenye shamba lake, linalojumuisha mabustani.

Fedha zikiwa nguzo kuu kufanikisha malengo ya karibu kila jambo hasa kwenye kilimo na biashara, Elizabeth anadokeza kwamba walianza kwa kuchanga kila wiki ili kupigana jeki wenyewe kwa wenyewe.

Aidha, walitumia mfumo wa mzunguko (Merry-go-round).

“Tulianza kwa kutoa Sh20, kisha 50, halafu baadaye Sh200 na sasa tumepanda, huchanganya Sh500 kila mwanachama kwa wiki,” anafafanua.

Kaunti ya Kitui ni tajika katika ukuzaji wa ndengu, mbaazi, mbegu za kunde na mahindi, na shabaha ya kundi hilo ni kulima mboga, hususan za kienyeji zinazoshirikisha mnavu almaarufu sucha au managu, mchicha – terere, na saga.

Isitoshe, wanalima sukuma wiki, spinachi na kabichi.

Elizabeth Kyalo, mwenyekiti wa muungano wa wajane Kitui, Wekwatio Self-Help Group, unaokuza mseto wa mboga na mimea mingine. PICHA|SAMMY WAWERU

Cha kutia moyo zaidi, Kitui ikiwa eneo kame, kwenye mabustani yao wamekumbatia mifumo ya kisasa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kama vile ‘mashamba ya ghorofa’ ndiyo conical na vertical gardens kwa Kiingereza.

Katika Kijiji cha Kalandini, Kaunti Ndogo ya Kitui ya Kati, Wekwatio Self-Help Group ina bustani maalum ambalo hutumika kutoa mafunzo kwa wanachama kuhusu kilimo bora na cha kisasa.

Kila Jumanne, kulingana na Mwenyekiti Elizabeth hukutana.

“Tumepokea mafunzo kibao kuhusu lishe bora na kuangazia gapu ya chakula kwenye jamii,” anaelezea.

Kimsingi, kwa sasa wanaweza kuzipa familia zao lishe bora na yenye virutubisho faafu kimadini.

“Awali, tulikuwa tukila tu bora tushibe.”

Kavutha Jimmy, 59, mwanachama mjane anamimimia sifa kundi hilo kwa kumfumbua macho.

Kavutha Jimmy, mwanachama wa Wekwatio Self-Help Group Kitui ambaye pia ni mwekahazina. PICHA|SAMMY WAWERU

“Mbeleni sikuwa najua madhumuni na maana ya chakula kilichoafikia virutubisho faafu. Kwa sasa, visa vya kupeleka watoto hospitalini vimepungua,” anakiri mama huyu wa watoto watatu.

Kavutha ndiye mwekazahina wa muungano huo wa wajane, ambaye anaendeleza kilimo kwenye ekari moja.

Kando na kukuza mahindi na mbaazi, analima kwa wingi mboga za kienyeji anazosema zimesaidia kuboresha afya ya familia yake.

Shukran kwa Shirika la United States Agency for International Development (USAID) kupitia mpango wake maalum, Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS), japo ulitamatika 2023, ulioinua Wekwatio na kuifumbua macho kuhusu kilimo bora na endelevu.

Isitoshe, kando na kukithi familia zao mahitaji muhimu ya kimsingi kupitia kilimo cha mboga, wanachama hao wanaendeleza ufugaji wa kuku.

Serikali ya Kaunti ya Kitui imewapiga jeki kwa mashine ya kusaga chakula, hatua wanayoridhia kwa kuwapunguzia gharama ya malisho ya madukani.

Muungano wa Wekwatio Kitui umekumbatia mfumo wa mashamba ya maghorofa kulima mboga. PICHA|SAMMY WAWERU