Habari Mseto

Nitawaongezea wabunge mishahara – Cherop

August 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMWEL OWINO

MISHAHARA ya wabunge huenda ikaongezwa tena na kuwazidishia wananchi mzigo wa ushuru wanaotozwa.

Mwenyekiti Mteule wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), Bi Lyn Cherop, Alhamisi alisema kuwa akiidhinishwa kushikilia wadhifa huo atafanya tathmini iliyopelekea wabunge kupunguziwa mishahara.

Bi Cherop ambaye aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuchukua mahali pa Bi Sarah Serem, aliambia kamati ya bunge inayosimamia Fedha na Mipangilio kwamba kuna mfumo wa kukata rufaa katika SRC ambao wabunge wanaweza kutumia kuwasilisha malalamishi yao iwapo wanaona hawakutendewa haki.

“Wabunge wana haki ya kusikilizwa sawa tu na vyama vingine vya wafanyakazi vilivyowasilisha malalamishi yao wakati tathmini ya utendakazi ilipofanywa,” akaambia kamati hiyo inayosimamiwa na Bw Joseph Limo.

Aliongeza: “Siwezi kusema kwamba wabunge wanalipwa kiasi kikubwa cha mishahara kupita kiasi lakini hayo ni maoni ya watu wengi, inahitajika pawepo mdahalo kuhusu suala hilo.”

Swali kuhusu mishahara ya wabunge na dhana kuwa wabunge hulipwa mshahara mkubwa kupita kiasi liliulizwa na Mbunge wa Alego Usonga, Bw Sam Atandi.

Bw Atandi alimtaka Bi Cherop aeleze wazi kile atakachofanya kuhakikisha kuwa uhusiano mbaya uliokuwepo kati ya SRC na wabunge kuhusu kukatiwa mishahara yao umetatuliwa.

Hata hivyo, Bi Cherop ambaye alisema ana utajiri unaofika Sh80 milioni, aliambia wabunge kuwa akiidhinishwa kushikilia wadhifa huo, ajenda yake kuu itakuwa ni kutatua gharama kubwa ya kulipa ushuru wa watumishi wa umma kwa ushirikiano na bunge, afisi ya rais na wadau wengine.

Mbunge wa zamani wa Rongo, Bw Dalmas Otieno, ambaye aliteuliwa kuwa kamishna wa tume hiyo alikosoa tume iliyoondoka kwa kudharau majukumu yanayotekelezwa na wabunge.

“Nilipoona SRC ikizungumzia majukumu ya wabunge, nilitambua hakuna kamishna yeyote aliyekuwepo ambaye alishughulika kutafiti kuhusu majukumu ya wabunge,” akasema Bw Otieno.

Alikosoa pia watu ambao wamekuwa wakifananisha wabunge wa Kenya na wa mataifa mengine akasema hali ya kisiasa humu nchini ni tofauti kabisa.

Huku akifichua kuwa utajiri wake unafika Sh320 milioni, alisema mahitaji ya wakazi katika maeneobunge huwa yanazidi kuongezeka ilhali mishahara ya wabunge hupunguzwa kila mara.

Katika utathmini wa mwisho wa mishahara uliofanywa, SRC ilitangaza kupunguza mishahara ya maafisa wakuu wa serikali akiwemo rais, madiwani na wabunge kuanzia Septemba mwaka uliopita ili kusaidia kuhifadhi Sh8.5 bilioni kila mwaka.