• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
Mafuta yaanza kusafirishwa tena baada ya makubaliano

Mafuta yaanza kusafirishwa tena baada ya makubaliano

Na BERNARDINE MUTANU

Shughuli ya usafirishaji wa mafuta imeanza tena kati ya Turkana na Mombasa. Shughuli hiyo ilianza Alhamisi baada ya kusitishwa kwa miezi miwili kutokana na maandamano makubwa Turkana.

Wakazi wa Lokichar, kunakotolewa mafuta walifunga barabara na kutatiza shughuli ya usafirishaji wa malighafi hiyo kwa kutaka kupewa nafasi za kazi na kuimarishwa kwa usalama eneo hilo.

Shughuli ya uchukuzi ilianza siku moja baada ya wakazi kuafikiana katika mkutano na viongozi wa eneo hilo.

Jumatano, Waziri wa Mafuta na Uchimbaji Madini John Munyes, Kamishna wa Kaunti ya Turkana Seif Matata, maafisa wa Kampuni ya Mafuta ya Tullow, wabunge James Lomenen (Turkana Kusini), Christopher Nakuleu (Turkana Kaskazini) na Mohammed Ali Lokiru (Turkana Mashariki) walifanya msururu wa mikutano katika maeneo ya Nakukulas, Lokichar na Kalemgorok na kuwarai wakazi kuruhusu usafirishaji wa mafuta kutoka eneo hilo hadi Mombasa.

Bw Munyes alisema serikali inatathmini mpango wa kubuni kamati itakakabiliana na malalamishi ambayo yameibuliwa na wakazi wa eneo hilo ili kuepuka changamoto kama hiyo siku zijazo.

You can share this post!

Washukiwa 9 wa Kenya Power wasakwa na DCI

Co-op kuwapa wateja mikopo ya Sh2 milioni kwa simu bila...

adminleo