• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
AFCON U-17: Uganda yafuzu kwa mara ya kwanza

AFCON U-17: Uganda yafuzu kwa mara ya kwanza

Na Geoffrey Anene

UGANDA imejiunga na Angola, Cameroon na wenyeji Tanzania katika Kombe la Afrika la soka ya wanaume wasiozidi umri wa miaka 17 mwaka 2019 baada ya kupepeta Ethiopia 3-1 katika mchujo wa Afrika Mashariki na Kati jijini Dar es Salaam, Agosti 26, 2018.

Waganda, ambao walianza mchujo huu uliovutia mataifa ya Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Djibouti, Sudan na Sudan Kusini kwa kulimwa 1-0 na Ethiopia mnamo Agosti 12, ililipiza kisasi kupitia mabao ya Idd Abdul Wahid (mawili) na Samson Kassozi. Ni mara ya kwanza kabisa Uganda imefuzu kushiriki kombe hili tangu lianzishwe mwaka 1995.

Uganda na Ethiopia zilikuwa katika kundi moja (B) na zilipiga Kenya 3-1 na 4-2 mtawalia katika kundi hili na kujikatia tiketi ya kushiriki nusu-fainali.

Waganda walicharaza Tanzania 3-1 katika nusu-fainali nao Ethiopia wakalemea Rwanda kwa njia ya penalti 4-2 baada ya muda wa kawaida kutamatika 2-2 Agosti 24.

Tanzania ilikamilisha kampeni yake kwa kulaza Rwanda kwa njia ya penalti 4-3 katika mechi ya kutafuta nambari tatu baada ya muda wa kawaida kumalizika 2-2.

Serengeti Boys ya Tanzania, ambayo ilibanduliwa nje ya Kombe la Afrika la mwaka 2017 katika mechi za makundi, ilifuzu moja kwa moja kushiriki makala ya mwaka 2019 kama mwenyeji.

Angola ilibwaga Afrika Kusini 1-0 katika fainali ya kusini mwa Afrika mnamo Julai 27 nchini Mauritius nayo Cameroon ikashinda Congo Brazzaville 3-1 katika fainali ya eneo la Afrika ya Kati mnamo Agosti 12 nchini Equatorial Guinea.

Tanzania itakaribisha mataifa saba nchini humo mnamo Mei 12-26, 2019. Morocco inahitaji sare pekee dhidi ya Tunisia hapo Agosti 28 kujinyakulia tiketi ya Afrika Kaskazini baada ya kuchapa Algeria 5-2 Agosti 20 na Libya 1-0 mnamo Agosti 24. Michujo ya kuamua wawakilishi watatu kutoka Afrika Magharibi itafanyika mwezi ujao wa Septemba.

You can share this post!

Yaibuka mashabiki wa #MashemejiDerby waliharibu mali ya...

Kikosi cha Gor kitakachosafiri Algeria chatajwa

adminleo