• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
SAKATA YA MAHINDI: Lesiyampe anyakwa na Haji

SAKATA YA MAHINDI: Lesiyampe anyakwa na Haji

Na PETER MBURU

MKONO mrefu wa sheria ambao majuzi umekuwa ukiwaangukia samaki wakubwa humu nchini Alhamisi umeelekea kwenye sakata ya mahindi ambapo wakulima walipoteza mabilioni ya pesa.

Hii ni baada ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuamrisha kukamatwa kwa maafisa saba katika bodi ya kuhifadhi nafaka nchini (NCPB) na Wizara ya Kilimo.

Bw Haji Alhamisi alielekeza kukamatwa na kushtakiwa kwa katibu katika Wizara ya Kilimo Richard Lesiyampe pamoja na maafisa wengine sita, kutokana na ununuzi haramu wa mahindi uliofanyika.

Maafisa hao wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa NCPB Newton Terer, Meneja Mkuu wa fedha Comel Kiprotich Ng’elechey, karani wa akaunti Caroline Kipchoge Cherono, Meneja wa behewa la Eldoret Renson Kibet Korir, afisa wa rekodi katika hifadhi ya nafaka ya Eldoret Eric Kipketer na Bw Joseph Kipruto, mkurugenzi wa kilimo kaunti ya Uasin Gishu.

Dkt Lesiyampe anatuhumiwa kuelekeza bodi ya NCPB kununua mahindi ikitumia bajeti ambayo haikuwa imeruhusiwa.

NCPB ilinunua mahindi hayo kwa niaba ya bodi ya kukagua ubora na utoshelezaji wa uhifadhi wa vyakula muhimu (SFROB) kwa miaka miwili kuanzia Oktoba 16, 2016.

“Baada ya uchunguzi, ilibainika kuwa NCPB ilitumia Sh11,365,879,918 hivyo ikizidi bajeti iliyotengwa ya Sh6bilioni. Bodi ya SFROB ilikuwa imepanga kununua magunia milioni mbili ya mahindi katika mwaka wa fedha 2017/18 kwa kutumia Sh6bilioni. Hivyo bajeti hii haikupangiwa na hivyo ni kinyume na sheria,” akasema DPP Haji.

Bw Haji aliongeza kuwa matumizi hayo hayakuzingatia kuwa ununuzi wa mahindi ulifanywa kulingana na sheria.

Washukiwa watashtakiwa kwa kukosa kufuata sheria inayohusiana na utumizi wa mali ya umma kimakusudi, kutumia pesa za umma kwa bila ruhusa, kushirikiana kupora, matumizi mabaya ya ofisi na kutelekeza kazi.

“Baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa hadi sasa na idhibati zilizopo, nimeelekeza tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) kuhakikisha kuwa washukiwa wanafikishwa kortini mara moja,” akasema Bw Haji.

NCPB bado inamulikwa kwa sakata ya kuwalipa wafanyabiashara Sh2bilioni kuwauzia mahindi mengi, huku wakulima wakikosa soko.

Sehemu ya taarifa rasmi ya DPP Noordin Haji aliyotundika katika akaunti yake ya Twitter Agosti 30, 2018.

You can share this post!

Kesi ya Mwilu yavutia wanahabari kutoka kona zote za dunia

Theresa May atua Kenya

adminleo