Mbuzi anaweza kutofautisha furaha na hasira kwa binadamu – Utafiti
Na PETER MBURU
Utafiti wa kusisimua umebaini kuwa mbuzi wana uwezo wa kutofautisha kati ya picha ya mtu anayecheka ama kutabasamu na yule aliyenuna, kisha wanachagua ya yule mwenye tabasamu.
Kulingana na utafiti huo, walipoonyeshwa picha mbili za mtu mmoja, moja ikiwa na uso wa tabasamu na nyingine ulionuna, mbuzi 20 wakufugwa katika utafiti huo walionyesha uwezekano mkubwa wa kuendea picha ya mtu anayetabasamu na kuigusa kwa mdomo.
Watafiti hao kutoka Uropa na Brazilia aidha walieleza kuwa mbuzi hao walichukua muda Zaidi karibu na picha za tabasamu, ikilinganishwa na zile zilizonuna.
“Mbuzi walikaa karibu na picha za nyuso za furaha kwa takriban sekunde 1.4, huku kwa picha za kununa zikikaa kwa sekunde 0.9,” ukasema utafiti huo wa chuo kikuu cha Queen Mary, London.
“Hiyo ni kumaanisha mbuzi wanatumia takriban asilimia 50 ya muda kushirikiana na picha za furaha, Zaidi ya picha za hasira ama huzuni.”
Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la Royal Society Open Science, na unadai kutoa dhibitisho la kwanza kuwa mbuzi husoma hisia za binadamu.
Utafiti huo ulihoji kuwa wanyama wa kufugwa wana akili zenye uwezo wa kusoma hisia kwenye mazingira na kubadili tabia kulingana na hisia za uso za binadamu.
“Utafiti huu una masuala ya umuhimu kuhusu jinsi tunashirikiana na wanyama wa kufugwa pamoja na wengine, kwa kuwa uwezo wa kusoma hisia za binadamu unaweza kuwa miongoni mwa wanyama wengi ila si wa kufugwa tu,” akasema Alan McElligott, mtafiti.
Timu hiyo aidha ilibaini kuwa mbuzi waliendea picha za nyuso zenye furaha hata walipowekwa mbele ya picha zenye hasira, wakisema wanyama hao hutumia sehemu ya kushoto ya akili kuibua hisia nzuri.