Habari

Mwanamume aandamana peke yake jijini kupinga bei ghali

September 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

KUZIDI kupanda kwa gharama ya maisha kumewasukuma Wakenya kujitokeza waziwazi na kumlilia Rais Uhuru Kenyatta kusuluhisha hali sasa, wakitumia kila aina ya mbinu kumfikishia Rais ujumbe.

Baada ya ushuru wa asilimia 16 wa VAT kuongezwa kwenye bidhaa za mafuta, mamilioni ya Wakenya wamebaki na kilio, kufuatia kupanda kwa bei za bidhaa za matumizi ya kimsingi kwa pesa nyingi.

Mwanamume mmoja Jumanne alipiga kambi nje ya jumba la Nation CentreJijini Nairobi akiwa amevalia ngozi na kubeba michongo ya watu na wanyama kama njia ya kupitisha ujumbe namna Wakenya wanavyoteseka.

Bw Jeremiah Kimotho alieleza Taifa Leo kuwa hatua yake ilichochewa na kuongezeka kwa vilio kutoka kwa wananchi masikini, ambao sasa wanamtaka Rais Kenyatta mwenyewe kuwaokoa kwa kuwa walimchagua kuwa kiongozi wao.

“Wanjiku ako na kilio, bei za bidhaa zimepanda, gharama ya maisha imeenda juu, Analia na amenituma niseme wezi warudishe pesa. Wanjiku asiitishwe pesa tena kutoka mfuko wake,” akasema Bw Kimotho.

Mzee huyo alisema Wakenya wanataka kuona wafisadi wakikamatwa na pesa walizoiba kurejeshwa kwa serikali kufanya kazi za kuendeleza nchi, kisha wafungwe jela.

“Pesa zilizoibiwa zikirudishwa, Wanjiku haaulizwa atoe pesa kutoka mfuko wake ili agharamie mahitaji ya serikali na ndio maana tunaunga mkono vita dhidi ya ufisadi,” akasema.

Alibeba michongo iliyochapishwa maandishi ya maovu yanayoendelea nchini akiorodhesha, mauaji, ufisadi, wizi, uongo na mengine.

“Hii nchi ina watu aina tatu ‘wadosi, hasla na masafara’, tunataka hata masafara wajiskie kuwa Wakenya. Tunataka kujisikia tuko kitu kimoja.”

Aliwasilisha ujumbe kwa Rais Kenyatta akitaka wezi wa mali ya umma wafungwe “tunataka kusikia wako jela hao wakubwa, sio mtu akiiba kuku analala kamiti leo, wakubwa wanalala kwao wakikula kuku.”