• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Niliumizwa kila sehemu ya mwili, Bobi Wine asimulia alivyoteswa

Niliumizwa kila sehemu ya mwili, Bobi Wine asimulia alivyoteswa

Na PETER MBURU

MWANASIASA na msanii wa Uganda Bobi Wine ambaye aliteswa sana na serikali ya Rais Yoweri Museveni alipokamatwa na kuzuiliwa na polisi na jeshi la nchi hiyo wiki chache zilizopita amesimulia visa vya kuogofya, kuhusu namna aliyoteswa na polisi na jeshi akiwa kuzuizini.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Bw Wine(ambaye jina lake kamili ni  Kyagulanyi Ssentamu) na ambaye ni mbunge wa Kyadondo alisimulia kuwa alikumbana macho kwa macho na watu wenye nyoyo za uhayawani na ambao walielekea kumwangamiza.

Akiorodhesha mateso aliyopokea, alisema maafisa waliomkamata walitesa nyeti zake, kumpiga kwa viatu na bunduki, licha ya kumyima chakula na haki za kimsingi, hadi akapoteza fahamu.

“Kila mtu alikuwa akinivamia kila mmoja wao akitafuta mahali pazuri pa kunijeruhi, siwezi kusema kwa kweli walikuwa wangapi lakini walikuwa wengi. Hakuna sehemu ya mwili wangu iliyosazwa walinipiga macho, mdomo na pua. Hao watu ni wanyama,” akasema Bw Wine.

Kwenye simulizi ya zaidi ya maneno 3,000 mwanasiasa huyo ambaye amekuwa upande wa upinzani wa Rais Museveni alishangaa namna serikali yake ingemtendea unyama wa aina ile raia wake.

“Walivuta nyeti zangu na kuzifinya wakitumia vifaa ambavyo sikuviona. Walinisukumia mateso ambayo siwezikumwombea yeyote kufanyiwa, hata Rais Museveni,” akaandika.

Vilevile, alieleza mazingira mabovu ambayo aliwekwa katika seli za kijeshi na polisi, namna alivyolazimishwa kutia saini karatasi ambazo hakujua zilikuwa za nini na kupewa ‘matibabu’ ambayo hakufahamu ni ya nini bila hiari yake.

Lakini alishukuru ulimwengu kwa kupiga kelele kuhusu kuzuiliwa kwake bila habari kutolewa na kuhusu malalamiko alipoteswa, akisema hali hiyo ilitia wasiwasi serikali na ikaanza kurudi nyuma katika hatua zake za kinyama.

“Ni kinaya kuwa maafisa wa seikali waliokuja kuniona walienda kutoa habari za kupotosha kwa umma kuwa hali yangu ilikuwa sawa. Na kelele zilipozidi ikawa wazi kuwa walitaka nitakapofika kortini nionekane mwenye afya bora. Mmoja wa maafisa nikiwa jela ya Makindye aliniambia nisipotumia dawa na kula vizuri kabla ya tarehe ya kufika kortini Agosti 23 serikali haingeruhusu wanahabari kuniona,” akasema Bw Wine.

“Alisema wangeniweka rumande hadi nifikie hali ‘nzuri kuonekana’. Hata walininyoa ndevu kwa nguvu.”

Lakini alisema vita bado vipo, akitaka ulimwengu kufahamu kuwa si maafisa wote wa polisi na jeshi wasio na utu, kwani kunao wanaotaka haki na uhuru wa kweli vipatikane Uganda.

Alimalizia kwa kusema kuwa atatoa habari kuhusu anachodhani sharti kifanyike Uganda ili kuendeleza vita vya kutafuta uhuru.

You can share this post!

Kopa Ruto tulipe deni la Sh5 trilioni, Wakenya wamshauri...

Ushuru zaidi waja – Ruto

adminleo