Simbas kumenyana na mahasidi Namibia Nairobi Oktoba 28
Na Geoffrey Anene
KENYA Simbas itaalika miamba Namibia jijini Nairobi hapo Oktoba 28 kwa mechi ya kirafiki kabla ya kuelekea nchini Ufaransa kwa mchujo wa mwisho wa kuingia Kombe la Dunia la raga ya wachezaji 15 kila upande utakaofanyika Novemba 11-23, 2018.
Kwa mujibu wa gazeti la The Star, Simbas ya kocha Ian Snook pia huenda ikajipiga msasa dhidi ya Ureno nchini Ufaransa kabla ya kukabiliana na Canada, Hong Kong na Ujerumani katika mchujo huo, ambao mshindi ataingia katika Kundi B linalojumuisha New Zealand, Afrika Kusini, Italia na Namibia.
Gazeti hilo limesema nyota wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Shujaa, Nelson Oyoo, Andrew Amonde, Dennis Ombachi na Samuel Oliech wameitwa kujiunga na Simbas baada ya majukumu na klabu zao kwenye duru ya raga ya kitaifa ya Dala Sevens mjini Kisumu hapo Septemba 8-9.
Kenya inafahamu Namibia vyema. Zimekutana mara 11 Simbas ikishinda mara mbili (30-26 mwaka 2006 na 29-22 mwaka 2014) na kupepetwa mechi zingine zote ikiwa ni pamoja na 53-28 zilipokutana katika fainali ya Kombe la Afrika mwezi uliopita wa Agosti.
Simbas imewahi kukutana na Ureno na Ujerumani mara moja pekee. Ilicharaza Ureno katika mechi ya kujipima nguvu mnamo Mei 30 mwaka 2015 uwanjani RFUEA jijini Nairobi. Simbas ilimenyana na Ujerumani mnamo Mei 27 uwanjani RFUEA na kuzabwa japo pembamba 30-29. Haijawahi kukutana na Canada katika raga ya wachezaji 15 kila upande.
Kenya na Hong Kong pia zinafahamiana sana. Mwaka 2017 pekee, zilikutana mara tatu. Hong Kong ilikaba Simbas 19-19 na kuipiga 43-34 mwezi Agosti jijini Nairobi kabla ya kuiongeza kichapo kingine cha 40-30 mjini Hong Kong mwezi Novemba.