Habari Mseto

Ajabu ya ng'ombe kuua simba zizini

September 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

SIMBA ambaye amekuwa akiua mifugo wa wenyeji karibu na Mbunga ya Kitaifa ya Meru aliuawa na ng’ombe Alhamisi usiku katika tukio lisilo la kawaida.

Simba huyo alifariki katika kijiji cha Luciuti, Amwathi, kaunti ndogo ya Igembe Kaskazini, alipojaribu kumla ng’ombe mwingine katika boma la mjane.

Diwani wa Amwathi Bw John M’Ngai, ambaye ng’ombe wake wawili waliangamizwa na simba huyo wiki jana, alisema mnyama huyo wa mwituni alifariki baada ya kunyongwa na kamba ya ng’ombe aliyekuwa akijaribu kumla.

Mlinzi wa Shirika la Huduma za Wanyama Pori (KWS), Bw Nathan Gatundu, alisema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kilichomuua simba huyo.

Inadaiwa njaa na mahangaiko ndizo zilimuua simba huyo.

Bw M’Ngai alisema simba huyo ambaye amekuwa akizurura vijijini usiku baada ya kutoroka mbungani, alifariki baada ya kunaswa katika mtego huku ng’ombe akifanikiwa kujiokoa kutoka kwa kucha zake.

“Simba aliingia katika boma la mjane huyo usiku wa manane na kufululiza hadi zizi la ng’ombe. Lakini alipokuwa aking’ang’ana kumla ng’ombe, alinyongwa na kamba iliyokuwa imefungwa shingoni mwa windo lake. Nadhani huu ni muujiza kwa sababu mjane huyo maskini alikuwa tu na ng’ombe huyo,” akasema.

Diwani aliongeza kuwa simba huyo ambaye amewaua mifugo kadha katika eneo hilo alivamia boma lake Ijumaa na Jumapili wiki jana.

Alieleza: “Aliua ng’ombe mmoja Ijumaa na mwingine Jumapili. Amekuwa akijificha vichakani wakati wa mchana ili kukwepa walinzi wa KWS na wakazi ambao wamekuwa wakimsaka.”

Bw Gatundu alisema uchunguzi wa awali ulibaini simba alikuwa amekula kitu kama ngozi ya mbuzi, lakini sampuli zaidi zimepelekwa kufanyiwa uchunguzi kubaini kiini.

Tukio hilo lisilo la kawaida liliibua msisimko mkubwa katika kijiji hicho ambapo wakazi hulalamikia visa vya uvamizi vya mara kwa mara kutoka kwa wanyapori wanaotoroka mbugani.