• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
#KenyaVsGhana: Mashabiki washenzi waonywa vikali

#KenyaVsGhana: Mashabiki washenzi waonywa vikali

Na Geoffrey Anene

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limetoa onyo kali kwa mashabiki wakorofi likiwataka wakae nyumbani wakati Harambee Stars ya Kenya itakuwa ikipepetana na Black Stars ya Ghana uwanjani Kasarani hapo Septemba 8, 2018 katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019.

Akizungumza na wanahabari katika uwanja wa Kasarani, Rais wa FKF Nick Mwendwa amesema amefurahishwa na mipango ya usalama iliyofanywa na idara ya polisi kuhakikisha usalama unadumishwa kabla ya mechi, wakati wa mechi na baada ya mechi.

“FKF imeridhika na mipango ya usalama ambayo imewekwa. Tuna uhakika kwamba tishio lolote la kiusalama litakabiliwa. “Tunaomba mashabiki waje uwanjani kwa utulivu, wasivuruge mechi. Wale wana nia ya kuvuruga mechi wasijaribu kukaribia Kasarani.

“Usalama utakuwa wa hali ya juu. Mechi ni ya kiwango cha juu (A) cha Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) kwa hivyo usalama utakuwa mzuri sana. Vikosi vya usalama vitakuwa tayari kukabiliana na hatari yoyote kesho (Jumamosi).

“Kuna vikosi vya GSU na vile vya mbwa wanaonusa. Maafisa wa polisi pia watavalia kama raia na kuwa ndani ya mashabiki. Hatutafanya mzaha na shabiki yeyote atakayejaribu kuharibu mechi.

Usalama katika meneo ya kuegesha magari pia utakuwa wa hali ya juu. Maafisa wa polisi wamekuwa wakijiandaa kwa mchuano huu kwa siku 10 niko na uhakika hatutashuhudia kisa chochote. Mtu yeyote atakayejaribu kuzua fujo atakabiliwa vilivyo. Atakamatwa na kutiwa rumande wikendi yote, na FKF pia itahakikisha amefikishwa kortini Jumatatu,” Mwendwa amesema.

Aidha, afisa huyu, ambaye alichaguliwa kuongoza FKF mwezi Februari mwaka 2016, ameomba mashabiki kujitokeza kwa wingi akiwahakikishia usalama wao na familia zao zitakazofika uwanjani. Ametaka mashabiki kununua tiketi zao katika duka la Kenya Cinema katikati mwa jiji la Nairobi.

Mashabiki pia wataweza kununua tiketi Jumamosi mkabala wa hoteli ya Safari Park kabla ya kuingia Kasarani ama kati milango nambari 4 na 12 katika uwanja wa Kasarani. Ameonya hakuna shabiki ambaye hatakuwa na tiketi ataruhusiwa kuingia uwanjani.

Afisa wa polisi anayesimamia kituo cha Kasarani Robinson Mboloi ametoa hakikisho kwamba usalama utakuwa shwari uwanjani Kasarani.

Ghana inaongoza kundi hili kwa alama tatu baada ya kulipua Ethiopia 5-0 mjini Kumasi mwaka 2018. Inafuatiwa kwa karibu na Sierra Leone, ambayo ilinyamazisha Kenya 2-1 jijini Freetown. Kenya na Ethiopia hazina alama. Timu mbili za kwanza kutoka kundi hili zitaingia AFCON mwaka 2019.

Vikosi:

Kenya:

Makipa – Patrick Matasi (Tusker), Farouk Shikalo (Bandari) na Ian Otieno (Red Arrows, Zambia);

Mabeki – Philemon Otieno (Gor Mahia), Jockins Atudo (Posta Rangers), Dennis Odhiambo (Sofapaka), Joash Onyango (Gor Mahia) Benard Ochieng (Vihiga United), Abud Omar (Cercle Brugge, Ubelgiji), David Ochieng’ (Brommapojkarna, Uswidi), Eric Ouma (Vasalund, Uswidi), Joseph Okumu (AFC Ann Arbor, Marekani), Musa Mohammed (Nkana, Zambia) na David Owino (Zesco United, Zambia);

Viungo – Francis Kahata (Gor Mahia), Abdallah Hassan (Bandari), Anthony Akumu (Zesco United, Zambia), Eric Johanna (Brommapojkarna, Uswidi), Ismail Gonzalez (Las Palmas Atletico, Uhispania) na Johanna Omollo (Cercle Brugge, Ubelgiji);

Washambuliaji – Piston Mutamba (Sofapaka), Jesse Were (Zesco United, Zambia), Michael Olunga (Kashiwa Reysol, Japan) na Ovella Ochieng (Vasalund, Uswidi).

 

Ghana

Makipa – Lawrence Ati (Sochaux, Ufaransa), Richard Ofori (Martizburg, Afrika Kusini);

Mabeki – Harrison Afful (Columbus, Marekani), Daniel Opare (Antwerp, Ubelgiji), Rashid Sumaila (Red Star Belgrade, Serbia), Daniel Amartey (Leicester City, Uingereza), Andy Yiadom (Reading, Uingereza), Nicholas Opoku (Udinese, Italia);

Viungo – Afriyie Acquah (Empoli, Italia), Isaac Sackey (Alanyaspor, Uturuki), Ebenezer Ofori (New York City FC, Marekani), Christian Atsu (Newcastle, Uingereza), Edwin Gyasi (CSKA Sofia, Bulgaria), Kwadwo Asamoah (Inter Milan, Italia), Frank Acheampong (Tianjin Teda, Uchina), Nana Ampomah (Waasland-Beveren, Ubelgiji);

Washambuliaji – Raphael Dwamena (Levante, Uhispania), Thomas Partey (Atletico Madrid, Uhispania), Majeed Waris (Nantes, Ufaransa) na William Owusu (Antwerp, Ubelgiji)

You can share this post!

Watumizi wa mafuta taa mijini sasa wageukia kuni kwa upishi

Mwendwa aahidi Harambee Stars donge nono wakiilima Ghana

adminleo