TAHARIRI: Wageni waheshimu ukarimu wa Wakenya
NA MHARIRI
KUFURUSHWA kutoka humu nchini kwa raia wa Uchina Liu Jiagi hapo Alhamisi kunaashiria uhusiano tata baina ya Kenya na Uchina.
Bw Liu alirekodiwa kisiri kwenye video na mafanyakazi Mkenya aliyetishiwa kutimuliwa kutoka duka la pikipiki la Mchina huyo.
Kwenye video hiyo, Liu anadai kwamba hakuna jambo ambalo Wakenya maskini, weusi na wanaonuka wanaweza kumfanyia kabla ya kumalizia cheche za matusi ambazo kibwagizo chake kilikuwa ‘Wakenya ni nyani.’
Ingawa tunafaa kuwa wakarimu na kuwaheshimu wageni katika taifa letu, viwango vya juu zaidi vya upigaji msasa vinafaa kuwekewa wanaosafiri Kenya kwa shughuli za kibiashara au kitalii.
Hakuna sababu ya mgeni yeyote kuja katika taifa letu na kuanza kututusi na kutubandika majina machafu.
Matusi ya ubaguzi wa rangi hayawezi kukubalika na Wakenya. Tunaiomba serikali kuhakikisha kuwa mikakati thabiti imewekwa ya kuwafungia wageni wenye hulka au nia mbaya.
Idara ya Uhamiaji inafaa kuwachunguza zaidi wanaowasilisha maombi ya leseni za kazi au biashara kutoka mataifa ya nje.
Athari za kuwakubalia wageni watundu wasio na shukrani kuingia humu nchini wakijiona muhimu zaidi kutuzidi sisi ni kuongezeka kwa visa vya ubaguzi kwa misingi ya rangi na kiuchumi.
Waama ni vigumu kuzuia matukio kama hayo kutokea hasa kwa sababu tu miongoni mwa taifa yenye changamoto nyingi.
Msimamo wetu ni kwamba kufurushwa kwa Liu kulikuwa hatua ya maana.Lakini mwenendo wake wa kijangili haufai kutufanya tuanze kuwachukia au kuwalaumu Wachina wengine wenye heshima wanaofanya biashara zao halali humu nchini bila kuvunja sheria.
Katika dunia ya sasa, hakuna taifa ambalo linaweza kujiengua kutoka kwa mifumo ya kilimwengu ya uhamiaji wa wanadamu wakisaka ajira. Lakini yeyote anayewadhalilisha Wakenya anafaa kukumbana na mkono wa sheria vilivyo na afunzwe kuwa Kenya ni nchi ya watu watiifu.
Tayari tuna matatizo yetu ya kibinafsi. Hatutaki mzigo mwingine kwenye mabega yetu. Kenya imeacha mipaka wazi kwa ulimwengu mzima kufanya biashara na kutalii.
Hatutaruhusu yeyote kuja hapa na kupuuza ukarimu wetu na kuuona kama udhaifu. Taifa tukufu kama letu linahitaji heshima nyakati zote.