Senegal vs Madagascar: Shabiki afariki kabla ya mechi
SHABIKI wa soka alifariki Jumapili huku wengine 40 wakinusurika na kupata majeraha mabaya kabla ya mchuano wa soka kati ya timu ya Taifa ya Madagascar na wapinzani wao Senegal katika uwanja wa Municipal de Mahamasina nchini Madagascar.
Mchuano huo uliomalizika kwa mabao 2-2 ulitanguliwa na msongamano wa maelfu wa mashabiki waliokuwa waking’ang’ania kuingia uwanjani kupitia lango moja ambalo lilikuwa likitumiwa kwa mauzo ya tiketi za mechi.
Vile vile wawili kati ya mashabiki wote 40 waliojeruhiwa wapo katika hali mbaya na wanaendelea kupokea matibabu katika mji mkuu wa Antananarivo.
“Tulikuwa tumepanga foleni na kusubiri tangu saa 12 asubuhi. Tulikuwa tumekaribia langoni watu walipoanza kuvutana na kung’ang’ania kuingia ndani. Japo nilikanyagwa mgongoni na kuumia, nilijizoazoa na kusimama,” akasema moja wa mashabiki hao Rivo Raberisaona akizungumza na Shirika la habari la AFP.
Shabiki mwengine, Henintsoa Mialy Harizafy ambaye mjomba wake aliumia katika purkushani hizo langoni alishangaa kwa nini shirikisho la soka nchini humo liliamua kutumia lango moja tu ingawa walifahamu vizuri umuhimu wa mechi na ushindani uliokwepo.
“Sielewi kwa nini walifungua lango moja tu ingawa walifahamu hii ilikuwa mechi kubwa,” akasema, Bw Henintsoa Mialy Harizafy.
Kufuatia sare hiyo, Senegal na Madagascar sasa zipo kileleni mwa kundi A kwa alama nne kila moja ingawa Madagascar wanadunishwa na idadi ya mabao.
Equitorial Guinea wanashikilia nafasi ya tatu huku Sudan wakiburura mkia bila alama yoyote katika mechi hizo za kufuzu kuwania ubingwa wa Afcon mwaka wa 2019.