VITUKO: Sindwele amfurusha Msodai nyumbani kwa Pengo kwa kukerwa na maudhi yake
NA SAMUEL SHIUNDU
MSODAI alipochapuka kutoka nyumbani mwa jiraniye Pengo, alibisha kwa Pengo. “Karibu ndani shemeji, naelekea madukani narejea.” Alikaribishwa na Felistus aliyezoea kumshemeji kila mtu. Msodai alifumwa na gere dhidi ya Pengo kwa bahati hii ya mke mzuri.
Msodai aliwakuta Pengo na Sindwele wakizungumza. Sindwele alimtazama mgeni huyu na akili yake ikamwambia kuwa aliwahi kuwona japo hakukumbuka ni wapi haswa walipoonana. ‘Haikosi tulikutana katika hizi lewa lewa zangu’ alijiambia akijaribu kukumbuka.
‘Lakini malevini wapi hasa? Huku Sidindi? La!’ aliendelea kujiuliza na kujijibu. Hakuwa na mazoea ya kulewa nje ya mipaka ya Maka. Alikuwa jogoo wa Maka ambaye hakudiriki kulewa Sidindi. ‘Potelea pote, itanisaidia nini nikijua tulikokutana?’ alijiambia hatimaye.
“Nimerejea kukujulia hali” Msodai alimjuza Pengo. Sindwele aligundua kuwa sauti ya mwanamume huyo haikubeba huruma hata kidogo. Akazidi kushawishika kuwa aliwahi kuisikia mahali fulani.
“Naona ungali tu ulivyokuwa tulipokuwa hapa” Msodai aliendelea kuroroja kwa sauti iliyobeba uchokozi na kero. Hakujua kuwa alikuwa anaupanda mchongoma ambao kuushuka ingekuwa noma. Sindwele hakumvumilia, “Hivyo sivyo mtu azungumzavyo. Kumbe hilo jichwa lako tupu?.” Alimuuliza.
“Kwani utado?” Msodai alimuuliza Sindwele kwa dharau. Sasa Sindwele alimkumbuka huyu mwanamume asiye na nidhamu. Waliwahi kukutana katika baa ya Jamhuri.
Alikumbuka jioni ile Pengo alipozindua kampeni za kuwania ukatibu wa chama cha walimu hapo baani Aliyakumbuka maneno ya bwana huyu yaliyobebwa na sauti la kilevi, ‘Pengo gani nazo zisizokwenda kwa daktari zikachopekwa meno?’ ndivyo alivyobwata mwanamume yuyu huyu jioni hiyo huko Jamhuri.
Sindwele alikumbuka jinsi mwanamume huyu alivyoapa kuwa hangempa Pengo kura hata kwa uchawi. Sasa alimfuma barabara kwa jicho la chuki. “Usiniangalie hivyo wewe!” Msodai alibwata
“Fanya heshima ndugu Msodai. Huyu ni rafiki yangu na hapa ni kwangu” Pengo alimkumbusha Msodai. “Usijali bwana Pengo. yaelekea amesahau kilichompata miaka mawili iliyopita .”Sindwele alikaulisha. Kwa hakika Pengo na Msodai hawakukumbuka hayo ya miaka mawili iliyopita.
“Akili yako imelegeza skrubu. Mimi sikujui wala sikumbuki lolote lililotukia miaka mawili iliyopita.” Msodai alijibu kwa takaburi. “Yangu imelegeza skrubu na yako ikakwenda mafyongo. Si wewe ndiye yule mlevi aliyetumwa na Kadenge kuuvuruga mkutano wa ndugu Pengo hapa. Umesahau ulivyonyanyuliwa vibaya vibaya na kufurushwa pakashume?” Sindwele alimkumbusha.
Msodai sasa alikumbuka yaliyompata. Sindwele akamshauri kuufyata na kuondoka au afurushwe kwa mara nyingine.
Msodai hakusubiri yafike huko. Akaondoka.