• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
KAULI YA MATUNDURA: Baraza la Kiswahili Kenya lahitaji kuungwa mkono kikamilifu

KAULI YA MATUNDURA: Baraza la Kiswahili Kenya lahitaji kuungwa mkono kikamilifu

NA BITUGI MATUNDURA

Mwezi uliopita, Baraza la Mawaziri la Kenya lilitoa idhini ya kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili Kenya (BAKIKE). Hatua hiyo ilizua msisimko miongoni mwa wapenzi, wakereketwa na wasomi wa Kiswahili.

Wadau wote wa Kiswahili walihisi kwamba hatua hiyo itazua mwamko mpya katika maendeleo ya Sera ya lugha kwa jumla, na hasa Kiswahili. Ingawa Kiswahili ni chombo muhimu cha mawasiliano katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati – na eneo la Maziwa Makuu ambapo lugha hii inazungumzwa na watu wasiopungua milioni 120, mataifa mengi hayana vyombo vya serikali vinavyoipigania lugha hii.

Mbali na Tanzania, hakuna nchi nyingine ambayo ina chombo rasmi cha serikali kinachoratibu maendeleo ya Kiswahili. Makataa ya kukamilisha mchakato wa kuundwa kwa Mabaraza ya Kiswahili katika nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa ni kufikia mwisho wa Agosti (mwaka huu). Kufikia sasa hatujaona Baraza la Kiswahili la Kenya likibuniwa.

Kisa na sababu ni kwamba mchakato wenyewe unaonekana kufanywa kwa mwendo wa kinyonga. Ingawa idhini ya Baraza la Mawaziri ya kubuniwa kwa asasi hiyo ilikuwa ni hatua nzuri, wasiwasi wangu ni kwamba mambo yote mazuri – hasa yanayolenga lugha husakamwa na matukio mengine nchini ambayo huelekea kupewa kipaombele.

Hali hii inazua mkururo wa maswali. Je, duru hii Kenya itafanikiwa kuunda chombo rasmi kitakachofadhiliwa na serikali katika kuongoza juhudi za ukuzaji na ustawishaji wa Kiswahili kimakusudi? Patakuwa na athari (z)ipi ikiwa Kenya itashindwa kwa mara nyingine kubuni asasi hii ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu?

Je, wabunge watachangamkia suala la kubuni na kupitisha miswada itakayofanikisha kubuniwa kwa chombo hiki haraka iwezekanavyo? Wadau wa Kiswahili wanapaswa kuchukua hatua gani kuhakikisha kwamba fursa ya kuwa na chombo hiki nchini Kenya haioitei vivi hivi tu?

Si rahisi kupata majibu ya maswali haya kwa misingi kwamba ubunaji wa Baraza la Kiswahili la Kenya ni suala la kisiasa kwa upande mmoja na suala la kisera kwa upande mwingine. Hii ina maana kwamba endapo halitaungwa mkono na kupata msukumo wa kutosha wa kisiasa, huenda mafanikio yakakosa kuafikiwa.

Kilichoko kwa sasa ni wataalamu wa Kiswahili, wakereketwa wa lugha hii, wadau wote kwa jumla kujitokeza wazi za kupigania kubuniwa kwa asasi hii kwa kila njia. Vyombo vya habari ambavyo vimenufaika kwa kutumia Kiswahili vinapaswa kuwa katika msitari wa mbele kutumia ulingo wao kuirai na kuidara serikali na wabunge ili waone umuhimu wa kubuniwa haraka kwa Baraza la Kiswahili.

Ikumbukwe kwamba, kuna manufaa mengi yatakayotokana pindi chombo hicho kitakapobuniwa. Kwa hiyo, ninatoa wito kwa idhaa za redio zinazotumia Kiswahili, magazeti – hususan Taifa Leo kuitumia kila fursa inayopatikana katika kupigania kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya.

Chama cha Kiswahili cha Taifa – Chakita, kinapaswa pia kuwa katika msitari wa mbele kuhakikisha kwamba fursa ya kubuniwa kwa asasi hiyo haipotei. Wala hakuna manufaa yoyote iwapo asasi hiyo itacheleweshwa kupatikana. Gogo haliendi ila kwa nyenzo.

You can share this post!

VITUKO: Sindwele amfurusha Msodai nyumbani kwa Pengo kwa...

Nilimtandika Zarika lakini majaji wakampa ushindi –...

adminleo