Bastola iliyopotea polisi akipambana na wauzaji bangi yapatikana
MWANGI MACHARIA NA RICHARD MAOSI
BASTOLA aina ya FA Ceska iliyopokonywa afisa wa polisi wiki mbili zilizopita hatimaye imesalimishwa katika idara husika Jumatatu katika eneo la Naivasha.
Mkuu wa Nyumba Kumi katika eneo hilo, Bw David Maina alisema kwamba alipata silaha hiyo hatari karibu na tanki ya maji, katika mtaa wa Matangini.
Hatimaye akaiwasilisha katika Kituo cha Polisi cha Karagita. Mbunge wa Naivasha Bi Jayne Kihara aliungana naye baadaye.
“Nilikuta bastola ndani ya mfuko wa plastiki, ndipo nikaamua kuipeleka katika kituo cha polisi,’’ Bw Maina alisema.
Mapema siku hiyo, Bi Kihara alikuwa ametoa makataa kwa yeyote aliyekuwa na bastola hiyo kuisalimisha mara moja, la sivyo angekumbana na mkono mrefu wa sharia.
“Nimefurahi kubaini kuwa mhusika aliitikia wito. Hii ni baada ya kutambua baadhi ya vijana walikuwa wameanza kukimbia makwao wakihofia adhabu kali kutoka kwa polisi waliokuwa wamewapa siku saba tu,’’ alisema Bi Kihara.
Afisa huyu alipoteza bastola katika harakati za kupambana na wauzaji bangi waliomzidia nguvu. Mapambano hayo yalimwachia afisa majeraha mabaya ya mikono huku matapeli wakitimua mbio.
Kuanzia siku ya tukio hilo, polisi walianzisha operesheni ya kusaka silaha hiyo hatari, isibaki mikononi mwa raia.
Kaimu mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Naivasha, Bw John Kwasa alithibitisha kwamba ni bastola hiyo iliyopotea kutoka kwa polisi ambayo ilipatikana.
“Silaha iliandamana na risasi 15 na huu ni mfano mzuri wa kuhimiza utendaji kazi wa Nyumba Kumi,” Bw Kwasa alisema. Hata hivyo aliwahakikishia wakazi kuwa polisi wataendelea kushika doria katika maficho ya wahalifu wakiahidi kuwaangamiza.