HabariSiasa

Harakisheni kuchunguza mauaji ya Sharon – Gavana Obado

September 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

PETER MBURU na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Migori Okoth Obado Jumatano alijitokeza kwa mara ya kwanza na kukanusha kuhusika na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno huku msaidizi wake Michael Oyamo akitokwa machozi kortini baada ya polisi kuruhusiwa kumzuilia kwa siku 14 zaidi.

Akihutubia wanahabari katika hoteli ya Serena jijini Nairobi, Gavana Obado alisema hajui chochote kuhusiana na mauaji hayo ya kinyama na kutaka vitengo husika kuharakisha uchunguzi ili wauaji kamili wajulikane.

“Kama mwananchi anayeheshimu sheria, ninataka kusema kinaga ubaga kuwa sikuhusika kwa vyovyote na mauaji ya kinyama ya Sharon,” akaongeza.

Gavana huyo alisema yuko tayari wakati wowote atakapohitajika kupeana habari zaidi ili wauaji halisi wa Bi Otieno wapatikane.

Gavana huyo alikosoa viongozi wa kisiasa na vyombo vya habari kwa kueneza kile alichosema ni kampeni ya kumchafulia jina ilhali hana makosa, huku akiwataka wasubiri uchunguzi ufanywe kubaini wauaji wa Sharon.

“Mauaji ya Sharon yalikuwa ya kushtua, ya kinyama na shutuma za umma dhidi yangu zimenyima familia yangu usingizi,” akaeleza.

Kiongozi huyo aliandamana na mkewe na wanawe wawili katika kikao hicho, pamoja na wakili wake Cliff Ombeta na baadhi ya maafisa wa Kaunti ya Migori.

Vilevile, Bw Obado alitoa rambirambi zake kwa familia ya marehemu, akisema pia naye ataridhika pale wauaji halisi watakapopatikana.

Wakati huo huo, polisi walikubaliwa kumzuilia kwa muda zaidi Bw Oyamo katika kituo cha polisi cha Muthaiga, Nairobi kwa siku 14.

Agizo hilo lilitolewa na Jaji Luka Kimaru aliyemjulisha Bw Oyamo kuwa tuhuma zinazomkabili za mauaji zina uzito mkubwa.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) anataka Bw Oyamo ashtakiwe kwa makosa ya kumuua Sharon usiku wa Septemba 3, 2018 katika eneo la Owade, Kaunti ya Homabay.

Jaji alimweleza mshukiwa kuwa hahitajiki kujibu shtaka hilo dhidi yake hadi polisi wakamilishe uchunguzi.

“Nakubaliana na kiongozi wa mashtaka kuwa wachunguzi wanahitaji kupewa muda wa siku 14 kukamilisha mahojiano na mshukiwa aliyetiwa mbaroni Septemba 4, 2018 kuhusiana na mauaji ya Sharon,” alisema Jaji Kimaru.

Ijapokuwa mawakili wanaomwakilisha mshukiwa huyo walipinga azuiliwe zaidi, Jaji Kimaru alisema wachunguzi wanahitaji kupewa muda kufanyia utafiti sampuli za DNA zilizotolewa kwa mshukiwa na wengine.

Mahakama ilisema utafiti wa kisayansi utakaofanywa ni sababu tosha ya polisi kuongezwa muda wa kukamilisha uchunguzi.

Hata hivyo alisema endapo polisi hawatakuwa wamekamilisha uchunguzi katika muda huo basi Bw Oyamo ataachiliwa huru.

Atakapokuwa rumande, Jaji Kimaru aliagiza watu wa familia yake na mawakili wakubaliwe kumtembelea.

Bw Oyamo atafikishwa kortini Septemba 25, mwaka huu.